August 26, 2016Wakati uongozi wa Klabu ya Simba ukitarajia kumfanyia uchunguzi zaidi beki wake, Hamad Juma ambaye alipasuka kichwani sehemu ya kisogoni kutokana na kuanguka bafuni, kuna lingine limeibuka jipya.

Hamad alipata jeraha hilo baada ya kuanguka bafuni na kuvuja damu nyingi hali iliyofanya akimbizwe Hospitali ya Mwananyamala jijini Dar, alipotoka alipewa wiki moja ya mapumziko ambapo aliamua kwenda nyumbani kwao kwa matibabu zaidi.

Lakini mara baada ya kutua Tanga juzi kufuatia kupewa ruhusa, uongozi umeshindwa kumpata kwa kuwa namba ya simu anayotumia haipatikani na mpaka kufikia jana jioni hawakuwa na taarifa zake zozote juu ya maendeleo yake.

Juhudi za kumpata hazikufanikiwa baada ya simu yake kuwa imezimwa muda wote, na alipopigiwa simu Meneja wa Simba, Mussa Mgosi naye alikiri kuwa hawajampata hewani mchezaji huyo.

“Tangu alipoondoka hatujampata hewani, nimempigia katika namba yake ninayoifahamu sijampata, lakini nitauliza kwa wachezaji wenzake kama kuna namba nyingine ambayo anatumia ili nijue maendeleo yake, si unajua tulimpa muda wa wiki moja kupumzika kama tulivyoshauriwa na madaktari? Hivyo nikipata taarifa zaidi nitakujulisha.”

Hamad alikutwa na tukio hilo siku moja tu baada ya mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Ndanda FC, ambapo alilazwa kwa siku moja hospitalini.

Mgosi aliongeza pia kuwa mpaka anaondoka kwenda Tanga, alikuwa anaendelea vizuri na kurejea uwanjani itategemea na ripoti ya daktari. 

Akimzungumzia mchezaji huyo, Daktari wa Simba, Yassin Gembe, aliliambia gazeti hili kuwa maendeleo yake ni mazuri na wanaamini baada ya wiki mbili atakuwa fiti kuanza mazoezi mepesi kwa ajili ya kujiweka sawa.


“Tumetoa muda huo kwa sababu hakupata matatizo makubwa kwenye ubongo pamoja na baadhi ya mifupa yake ya kichwani zaidi ya ile kupasuka pekee na kupoteza damu jambo ambalo kitaalamu halina athari sana na mara baada ya muda huo tuliompa atakuwa sawa,” alisema Gembe. 

2 COMMENTS:

  1. JAMAA KAENDA MUHEZA SEHEMU MOJA INAITWA PANDE(NYANZANI) KWA AKINA MWENDAMBIO KUSHUGHULIKIA MWILI WAKE,KWANI PALE SIMBA SI PAKUCHEZA BILA MWILI WAKO KUKOMAA.HIVYO ATAKAPOMALIZA TIBA,MZEE MBARUK ZUBER ATAMSINDIKIZA HADI DSM NA NDIO MTAPOONA SASA JAMAA ATAKAVYOCHEZA FULBACK KWA KISHINDO NA HAO AKINA MALIKA WATASUGUA BENCHI HADI WATATAMANI KUHAMA TIMU.

    ReplyDelete
  2. Mmmmmmmmh, ndugu una uthibitisho?

    ReplyDelete

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV