Baada ya Yanga kutolewa kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, kocha wa timu hiyo, Hans van Der Pluijm, ameeleza kuwa anataka kurejesha furaha kwa mashabiki wa timu yake kwa kuifunga African Lyon na kuchukua pointi zote tatu katika mchezo wao huo wa kwanza wa Ligi Kuu Bara, keshokutwa Jumapili.
Kocha huyo raia wa Uholanzi amesema anafahamu wana muda mchache wa maandalizi ya mchezo huo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam lakini hiyo haitawasumbua kwa kuwa tayari walishafanya maandalizi hayo kwa kutumia baadhi ya michezo ya kimataifa.
“Nafahamu kuwa mashabiki wanahitaji furaha na hakuna njia nyingine ya kuirejesha zaidi ya kuanza kwa kufanya vizuri kwenye mechi za Ligi Kuu Bara.
"Tumetolewa katika michuano ya kimataifa, hii ina maana kwamba moja kwa moja tunaelekeza akili na nguvu zetu ligi kuu, ushindi ni lazima.
“Kwa sasa tumebakiza siku chache za maandalizi lakini hiyo haitasumbua sana kwa kuwa tulishaanza maandalizi kwa kutumia mazoezi na mechi za michuano ya kimataifa. Wachezaji wengi tuliowakosa hivi karibuni, wameanza kurejea na mpaka siku hiyo, tutakuwa kamili,” alisema Pluijm.
Aidha, Pluijm aliongeza: “Mara baada ya kumaliza mechi ya mwisho dhidi ya TP Mazembe, nilifanya kikao na wachezaji kwa ajili ya kuwatengeneza kisaikolojia ili tutakaporejea kwenye ligi kuu, turudi na nguvu zote katika kulitetea taji hilo.
“Hivyo, hatutaki utani wala kudharau timu yoyote inayoshiriki ligi kuu, zikiwemo zilizopanda daraja, tuhakikishe tunautetea ubingwa wetu tunaoshikilia.”
0 COMMENTS:
Post a Comment