HANS POPPE |
Ikiwa ni siku chache baada ya Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji kumtaka beki Hassan Kessy kuondoa hofu kwa kuwa siku itafika atacheza, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe amesema huenda beki huyo akaendelea kubaki nje ya uwanja kwa msimu huu na mwingine.
Manji alisema hayo juzi huku akisisitiza, Kessy hawezi kutocheza milele.
Lakini Hans Poppe amesema kinachomponza Kessy ni ujeuri wa viongozi wa Yanga ambao wanajua wamekosea, lakini wanataka kuonyesha umwamba.
Akifanya mahojiano na SALEHJEMBE jijini Dar es Salaam, Hans Poppe amesema Yanga wanajua wamefanya makosa, lakini wanataka kuonyesha umwamba kama walivyozoea.
“Waliwahi kutufanyia hivi katika suala la Yondani, safari hii wamerudia na kumsainisha Kessy wakati akiwa bado na mkataba na Simba.
“Kama hiyo haitoshi, mkataba wameufikisha TFF, wameusajili na wakatuma Caf. Sasa sisi tuna kila kitu na ushahidi mwingine wao wenyewe wameupeleka TFF na Caf.
“Kilichotakiwa ni kuandika barua, nilikutana na Chanji (kiongozi Yanga). Nikamweleza andikeni barua mimi nitalisimamia hilo. Lakini hakufanya hivyo, wanataka kuonyesha ujeuri.
“Kama itaendelea hivi, ninaamini Kessy hatacheza. Na hapa wa kulaumiwa ni wao maana Simba tupo hapa,” alisema Hans Poppe na alipoulizwa kama wakiandika barua basi mara moja watamruhusu Kessy, akajibu.
“Wakiandika barua, basi sisi tuna jibu au majibu ya kuwapa. Sasa yatapatikana kutokana na barua yao.”
0 COMMENTS:
Post a Comment