August 12, 2016



Kama mchezaji umebahatika kuingia kwenye kikosi cha kwanza cha Mcameroon, Joseph Omog ndani ya Simba basi unatakiwa kupambana kwani ukizingua tu, benchi litakuhusu.

Hiyo ni kauli ya Kocha Msaidizi wa Simba, Mganda, Jackson Mayanja, aliyoitoa mara baada ya mchezo wa kirafiki na AFC Leopards ambapo Simba ilishinda kwa mabao 4-0.

Lakini wakati msaidizi akisema hivyo, bosi wake, Joseph Omog amewapa masharti magumu wachezaji wa kimataifa akiwemo Mrundi Laudit Mavugo kwa kuwambia ole wake atakayekaa benchi.

Omog amesema kuwa hakuna mchezaji wa kimataifa ambaye atakaa benchi kutokana na kuonyesha uwezo mdogo, badala yake kila mmoja anatakiwa ajitume ili aweze kupata nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza.

“Usajili nilioufanya unaendana na uhitaji wa kikosi changu na nimesajili wachezaji wa kimataifa kwa kuangalia kila mmoja anakuwa na kiwango na kila mmoja nahitaji acheze labda itokee mtu awe anaumwa kwani mchezaji wa kimataifa anatakiwa awe na uwezo zaidi ya wazawa.

“Kwa sasa bado sijapata kikosi cha kwanza japokuwa kuna baadhi ya wachezaji wanaonyesha kuwa na kiwango kizuri cha kucheza katika kikosi cha kwanza. ambaye atakaa benchi kutokana na kuonyesha uwezo wa chini huyo atakuwa hatufai,” alisema Omog.

Wachezaji wa kimataifa waliopo Simba ni Vicent Angban, Mavugo, Juuko Murshid, Musa Ndusha, Janvier Bokungu, Fredrick Blagnon na Method Mwanjale.

Upande wa Mayanja alisema usajili wao walioufanya chini ya Omog umekidhi viwango walivyokuwa wanavihitaji kwa ajili ya kuleta ushindani wa namba.

Mayanja amesema msimu uliopita hawakuwa na kikosi bora kwa ajili ya ushindani, hasa kwa wachezaji waliokuwa wakianza kikosi cha kwanza na wale waliokuwa benchi lakini sasa wanajivunia ushindani mkali ambao wanaamini utawasaidia kufanya vizuri.

“Yapo matarajio makubwa kwa mashabiki wa Simba kuuchukua ubingwa wa ligi kuu msimu ujao, kujiamini huko kunatokana na uwezo wa mchezaji mmojammoja ambao upo juu.


“Hivi ndivyo timu inavyotakiwa kuwa, lazima wawepo wachezaji watakaoleta ushindani, wale wanaokuwa benchi na wanaokuwa uwanjani wanacheza, wote uwezo wao unatakiwa kuwa sawa, kukosa hali hiyo kulichangia kutunyima ubingwa msimu uliopita,” alisema Mayanja.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic