August 31, 2016

KICHUYA, AKILIMILIKI MPIRA KATIKATI YA MABEKI WA JKT RUVU

Kocha Mkuu wa Simba, Mcameroon, Joseph Omog, amebadili mbinu za ufungaji mabao huku akiwatumia mawinga na mabeki wake wa pembeni kuanzisha mashambulizi.

Hiyo ni siku chache tangu timu hiyo itoke suluhu na JKT Ruvu kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa wikiendi iliyopita katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Safu ya mawinga ya timu hiyo inaundwa na Shiza Kichuya na Jamal Mnyate huku mabeki wa pembeni wakiwa ni Mohammed Hussein Zimbwe Jr na Malika Ndeule.

Omog alisema amepanga kutumia mipira ya pembeni katika kuanzisha mashambulizi baada ya mechi ya JKT Ruvu kupata ugumu wa kupenyeza mipira katikati kutokana na uimara wa safu ya ulinzi ya wapinzani wake.

Omog alisema, anaamini hiyo ni njia sahihi kwake katika upatikanaji wa mabao mara watakapokutana na timu inayocheza kwa kulinda lango lao wakati wote kwa kujazana wachezaji wengi nje ya 18.

Mcameroon huyo alisema, mechi ya JKT Ruvu walipata ugumu wa kufunga kutokana na wapinzani wao kucheza soka la kujilinda muda wote kwa kujazana langoni mwao.

Aliongeza kuwa, tayari ameanza kuwandaa mawinga na mabeki wake wa pembeni kwa kuwapa mbinu mbalimbali za jinsi ya kushambulia kwa kupiga krosi safi zitakazofika kwa washambuliaji wake wenye maumbile makubwa, Laudit Mavugo na Frederick Blagnon kwa ajili ya kufunga kwa kupiga vichwa.

"Kama ulivyoona katika programu ya mazoezi ya mwisho tuliyoyafanya kwenye Uwanja wa Boko Veterani siku moja kabla ya mechi hii ya JKT Ruvu, uliona jinsi nilivyokuwa nikiwaelekeza mabeki wa pembeni na mawinga wangu wanavyotakiwa kupiga krosi na kona zitakazowafikia washambuliaji wangu huku nikiwataka kufunga kwa kichwa.

“Kikubwa ninataka kuona tunatafuta mbinu nyingine mbadala za kufunga mabao kwa kutokea pembeni kwa mabeki na mawinga kupiga krosi hizo nzuri na siyo kulazimisha kufunga kwa kupenya katikati.

“Mfano uliona mechi na JKT Ruvu walijazana mabeki wengi katikati na kusababisha tushindwe kupenya kwa kupenyeza mipira kwa washambuliaji kutokana na rundo la mabeki, hivyo nimejaribu mbinu hiyo nyingine ya kutafuta mabao kwenye goli la timu pinzani, nafikiri nitaitumia kwenye michezo kadhaa ijayo nione kama ina mafanikio,” alisema Omog.


Amog amekuwa na staili hiyo ukiwa ni mwezi mmoja tu umebaki kabla ya mchezo wa watani wa jadi, Simba na Yanga Oktoba Mosi.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic