August 30, 2016



Na Saleh Ally aliyekuwa Madrid
UKIFIKA katika Jiji la Madrid, moja ya vivutio vikubwa ni majengo manne marefu zaidi katika jiji hilo, maarufu kama Cuatro Torres Business Area (CTBA).

Niliyashuhudia majengo hayo yako katika eneo la Paseo de la Castellana, pembeni kidogo tu mwa Jiji la Madrid na ndiyo majengo marefu zaidi nchini Hispania, yakiwa pia katika 10 bora ya majengo yote marefu zaidi ya Jumuiya ya Ulaya.

Niliamua kufuatilia kwa ukaribu kwa lengo la kujifunza, pia kujua mengi ambayo nitazungumza na wasomaji wa Championi kwa lengo la kuelezana namna wenzetu wanavyopambana katika upigaji hatua kimaendeleo na si maneno mengi tu.

Majina ya majengo hayo manne ni Torre Espacio ndiyo refu zaidi jijini Madrid na Hispania kote. Linashika nafasi ya tatu kwa urefu kwenye Jumuiya ya Ulaya baada ya England kujitoa kwenye jumuiya hiyo.


Mengine ni Torre de Cristal, Torre PwC na Torre Cespa. Sehemu hii ni kwa ajili ya ofisi pamoja na masuala mbalimbali ya kibiashara kama ofisi na mambo mengi yanayohusiana na uendeshaji wa biashara mbalimbali.

Wakati kuna majina hayo ya majengo yenyewe, wakazi wa Jiji la Madrid wao wanayatambua kwa majina yao ambayo ni majina ya nyota wa zamani wa Real Madrid ambao ni Zinedine Zidane, Ronaldo di Lima, Luis Figo na David Beckham.

Unaweza kushangazwa majengo hayo kujulikana kwa majina ya wachezaji wa Madrid, lakini ukweli ni hivi, yalipo ndiyo ilikuwa sehemu ya uwanja wa mazoezi wa klabu tajiri zaidi duniani ya Real Madrid. Wakati huo sehemu hiyo ikijulikana kama Ciudad Deportiva.

Mwishoni mwaka 2003, Rais wa Real Madrid, Florentino Perez, aliamua kuliuza eneo hilo kwa wawekezaji waliokuwa wamejichanga na kuhamishia sehemu ya mazoezi ya Madrid katika eneo la Valdebabas ambalo liko nje zaidi ya Jiji la Madrid.

Kwa uamuzi wake wa kuliuza eneo hilo, Real Madrid ilipata kipato kikubwa cha euro milioni 480 (zaidi ya Sh bilioni 950). Ambazo zilitumika katika ununuzi wa eneo la Valdebebas ambalo pamoja na kuwa kubwa kuliko maeneo yote ya michezo yanayomilikiwa na klabu duniani, Madrid hawajatumia hata nusu ya eneo hilo hadi sasa.


Lakini si kwamba fedha hizo zilisaidia kununua eneo hilo, badala yake ndiyo mwanzo wa kuanzishwa kwa Galacticos ambayo ilichangia kukua zaidi kwa umaarufu wa Real Madrid na kuchangia mafanikio makubwa kibiashara.

Wakati Perez amepata wazo la kuanzishwa kwa Galacticos alijua kwamba anatakiwa kusajili watu maarufu zaidi, wanaokubalika kutoka katika nchi mbalimbali barani Ulaya na kuwakusanya pamoja, wacheze soka, wabebe makombe na Madrid kuendelea kushika soko la soka duniani kote.

Luis Figo ambaye tayari alikuwa Barcelona, tayari alikuwa mradi kutoka kwao Ureno na Barcelona alipokuwa, lazima mashabiki wa Real Madrid wangemfurahia sana.

Zinedine Zidane tayari alikuwa ana soko kubwa kwao Ufaransa pia Italia akiichezea Juventus kwa mafanikio makubwa. David Beckham alishika soko la England lakini nchi za Asia na Afrika pia akiwa na Manchester United.


Halafu alikuwa na straika mfalme, huyu ni Ronaldo di Lima kutoka Brazil lakini akiwa ameanzia Uholanzi na PSV, akaenda akatamba Hispania akiwa Barcelona, Italia. Lakini alikuwa maarufu zaidi duniani. Hivyo ni soko jingine kubwa na uwezo wake pia ulikuwa ni mchango.

Hivyo Perez aliangalia mchango kwa maana ya uwezo na soko. Akawajumuisha wakali hao na kweli mafanikio makubwa sana yakapatikana.

Haikuwa rahisi kwa Perez kuonekana alikuwa akifanya kitu cha maana kwa kuwa Valdebebas ni eneo la nje zaidi ya Jiji la Madrid. Hivyo kuipeleka timu hiyo kubwa nje ya mji, tena ikiwa inabeba jina la mji huo ilionekana ni kosa kubwa, akapingwa hata na waliokuwa wasaidizi wake.

Alichofanya yeye ni kuwa alivyo sasa, kila aliyeona hakubaliani naye, basi alimtimua na kusisitiza hawezi kufanya kazi na watu wanaomvuta nyuma ndani ya klabu anayotaka isonge.

Kumekuwa na taarifa kwamba, bado Madrid inaingiza kiasi cha fedha kila baada ya miezi kadhaa kupitia eneo hilo, ingawa linaonekana ni kama jambo la siri sana.

Lakini leo, Madrid ina eneo kubwa zaidi ambalo pamoja na kujenga viwanja 13 vya soka, hoteli na ofisi, lakini bado halijatumika hata nusu yake na tayari watu wengi wamejenga kulizunguka eneo hilo lililo karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Barajas.

Ujenzi katika eneo la Valdebebas umekuwa ghali kwa kuwa watu wengi wameamua kujenga katika eneo hilo karibu na sehemu hiyo maarufu mji wa michezo wa Real Madrid, wenyewe Wahispania wanasema Ciudad Real Madrid.


Perez ndiye anaaminika kuwa kiongozi mahiri na jasiri kuliko wote katika mpira nchini Hispania. Pamoja na kwamba anamiliki fedha nyingi kwa kuwa ni mfanyabiashara mkubwa, lakini nguvu zake amewekeza katika maendeleo ya klabu hiyo.

Kwa sasa ni maarufu hata kuliko viongozi wote wa Serikali ya Hispania. Hii yote inatokana na ujasiri wake na ule uamuzi wa kulenga kupata mafanikio bila ya kuogopa wanaompinga.

Huenda Hassan Dalali anaweza kupata hata asilimia tano ya Perez kwa kuwa aliamua ununuzi wa uwanja wa mazoezi wa Simba kwa kununua eneo Bunju na sasa Simba wameendelea kujenga uwanja wao wa mazoezi.
Lakini bado kuna viongozi wengi wanapaswa kuendea huko. Real Madrid bado ni timu inayomilikiwa na wanachama. Lakini ni wale wanaoheshimu viongozi wenye uamuzi sahihi wa kutaka kuleta maendeleo.

Kupitia Perez, Madrid iliuza eneo dogo, ikanunua kubwa ambalo sasa lina thamani kubwa. Lakini ikajiimarisha kibiashara kwa kuwasajili nyota kutoka nchi mbalimbali za Ulaya na kufanikiwa kuongeza umaarufu na ubora wa biashara yake katika masoko mbalimbali ndani ya Hispania, Ulaya na duniani kote.

Maamuzi magumu, yenye ndoto sahihi kupitia mipango thabiti ni chachu ya mabadiliko kama Madrid walivyofanya mabadiliko kutoka katikati ya jiji hadi Valdebebas.




0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic