August 1, 2016


Yanga ikiwa inatafuta ushindi kwa udi na uvumba katika mechi yake inayokuja dhidi ya Waarabu wa Algeria, MO Bejaia, imejikuta ikimpoteza na kushindwa kumtumia straika wake hatari, Mzimbabwe, Donald Ngoma.

Yanga itashindwa kumtumia mshambuliaji wake huyo aliyefunga mabao manne mpaka sasa katika michuano hiyo ya Kombe la Shirikisho Afrika kutokana na adhabu ya kadi mbili za njano ambayo kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Afrika (Caf), mchezaji anapaswa kukosa mchezo unaofuata.

Ngoma alipata kadi ya pili katika mchezo wao dhidi ya Medeama uliopigwa nchini Ghana na kufungwa kwa mabao 3-1. Mwingine aliyepata kadi katika mchezo huo ni Nadir Haroub ‘Cannavaro’, yeye atacheza dhidi ya Bejaia lakini anapaswa kujichunga asipate nyingine ya pili.

Kutokana na hilo, Kocha wa Yanga, Hans van Der Pluijm, amesema Ngoma ni mchezaji muhimu lakini kwa kuwa ana kikosi kipana hakuna tatizo katika hilo, ataiziba nafasi hiyo siku hiyo na kila kitu kitakwenda sawa.

Yanga inatarajia kuvaana na Bejaia Agosti 13, mwaka huu, katika Uwanja wa Taifa, siku ambayo pia Mwanamuziki wa Tanzania, Fareed Kubanda ‘Fid Q’ atakuwa anasherehekea siku yake ya kuzaliwa.

“Katika mechi ya Bejaia nitamkosa Ngoma tu kutokana na kadi mbili za njano alizonazo, kweli ni mchezaji mzuri lakini kwa kuwa nina kikosi kipana hapa, hakuna kitakachoharibika, tutawatumia waliopo kwa ajili ya kuipigania timu,” alisema Pluijm, raia wa Uholanzi.

Katika michuano hiyo, hii ni mara ya pili, Ngoma anakaa nje kutokana na adhabu ya kadi mbili za njano, awali alikosekana katika mechi iliyopigwa Uwanja wa Taifa, Dar dhidi ya Cercle de Joachim ya Mauritius.




0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic