AGYEI |
Baada ya Azam FC kufanikiwa kunasa saini ya mshambuliaji wa Medeama ya Ghana, Enock Atta Agyei, Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van Der Pluijm, anayemfahamu vizuri kijana huyo, amefunguka kuhusiana na uwezo wake na jinsi gani Azam imelamba dume katika maamuzi yake hayo.
Akiwa na Medeama, Agyei alifanikiwa kulishawishi benchi la ufundi la Azam kwa kuonyesha soka la ushindani na usumbufu mkubwa kwa wapinzani wao Yanga SC, walipoumana Uwanja wa Taifa, Dar wiki mbili zilizopita katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Pluijm, mwenye makazi yake nchini Ghana, amesema Azam wamepata mchezaji mzuri na anamfahamu kuwa ni mtu asiyetaka kushindwa, mwenye uchu wa mafanikio lakini kuhusu matokeo yake uwanjani pia itategemea Azam wamepanga kumtumia vipi.
“Unajua huyu jamaa ni mchezaji wa Azam sasa, hivyo nisingependa kumzungumzia sana lakini kwa kifupi ni mchezaji mzuri, anajua anafanya nini uwanjani, mwenye kutaka kufanikiwa muda wote na ana uchu kwa kile anachokihitaji muda huo.
“Pale Ghana ninawafahamu vijana wengi sana ambao kwa sasa ni tegemeo kwenye vikosi mbalimbali na huyu Agyei pia ni mmojawao lakini itategemea na Azam wenyewe wamepanga kumtumia vipi, ila kwa kifupi ni mtu mzuri na Azam wamepata mchezaji,” alisema Pluijm.
Kuhusiana na mchezo wao dhidi ya Azam wa Ngao ya Jamii utakaopigwa Agosti 17, mwaka huu, kocha huyo raia wa Uholanzi alipoulizwa kuhusiana na usumbufu wa uwanjani wa mchezaji huyo na amepanga kumdhibiti vipi, alifunguka kama ifuatavyo:
“Hapana, timu si mchezaji mmoja, huwezi kuandaa timu kwa ajili ya mchezaji mmoja, soka ni mchezo wa muungano na Azam ni timu nzuri kwa hiyo utahitaji kuiandaa timu kwa ajili ya mbinu za kucheza na maeneo husika ya wapinzani lakini si mchezaji mmoja.”
0 COMMENTS:
Post a Comment