August 1, 2016


Katika kuhakikisha wachezaji wa Simba wanakuwa na stamina ya hali ya juu, kocha wa kikosi hicho, Joseph Omog, jana asubuhi aliamua kuwakimbiza wachezaji wake kwenye milima kwa takriban dakika 30.

Mazoezi hayo ya jana Jumapili, yalianza saa 2:00 na kumalizika saa 4:15, yalianzia uwanjani, kisha wakahamia milimani kabla ya kurudi tena uwanjani kumalizia programu ya asubuhi.

Katika mazoezi hayo mwanzo mpaka mwisho wachezaji walianza kwa kunyoosha misuli na kuchezea mpira kwa saa moja, kabla ya kuelekea milimani.

Katika zoezi la kukimbia milimani, Kocha Mkuu Joseph Omog aligawa makundi mawili ambapo kundi moja aliliongoza yeye huku lingine likiongozwa na msaidizi wake, Jackson Mayanja.

Zoezi hilo lililodumu kwa takriban dakika 30, lilikuwa rafiki kwa wachezaji wote kwani hakuna hata aliyetegemea wala kulalamika kuchoka huku wakionekana kuwa na ari kubwa ya mazoezi.

Baada ya hapo, wakarudi uwanjani kumalizia dakika 45 kwa kuchezea mpira.


Omog ameyazungumzia mazoezi hayo ya milimani kwa kusema: “Ni maalum kwa ajili ya kuongeza pumzi, stamina lakini pia ni mazuri kwa kunyoosha misuli baada ya wiki nzima kucheza uwanjani pekee. Kikubwa wachezaji wangu wanaonyesha ushirikiano mzuri kwa kila zoezi.”

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV