August 16, 2016
Na Saleh Ally
BAADA ya kukamilika kwa zoezi la usajili la kikosi cha Simba, timu yake ilicheza mechi kadhaa za kirafiki na kuonyesha mwelekeo.

Mechi nne za mwanzo ambazo Simba ilishinda tatu na kupoteza moja, zote zilikuwa dhidi ya timu za daraja la kwanza.

Mechi ya tano ilikuwa dhidi ya AFC Leopards ya Kenya, moja ya timu kongwe katika Ukanda wa Afrika Mashariki. Simba ilishinda kwa mabao 4-0 huku ikionyesha kiwango bora kabisa mbele ya mashabiki wake waliojitokeza kwa wingi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe ambaye pamoja na wenzake walishirikiana na Kamati ya Ufundi ya Simba kufanya usajili huo, anaamini kikosi chao kipo vizuri.

Katika mahojiano na SALEHJEMBE, Hans Poppe amesema anaamini Simba imekaa vizuri lakini kuna mambo kadhaa ya kufanya kwa ajili ya mwendelezo ili kikosi hicho kimalize ligi kikiwa na makombe mkononi.

SALEHJEMBE: Dirisha la usajili limefungwa, maana yake kazi ya usajili imekamilika. Vipi mwenyekiti umeridhika na kikosi chako?
Hans Poppe: Kwa maana ya muunganiko wa kikosi, timu ni nzuri.

SALEHJEMBE: Msimu uliopita, Simba ilionekana nzuri kwenye kuanza, lakini walio benchi hawana makali, mmelifanyia kazi hilo?
Hans Poppe: Kweli huko nyuma tulionekana na tatizo hilo, tulipocheza na AFC Leopards ilionekana tatizo limetatuliwa. Wachezaji 11 ndani na 11 nje, maana yake kuna uhakika.


SALEHJEMBE: Katika hili mmehusisha suala la ufungaji, maana mlionekana mmesimamia mguu mmoja msimu uliopita?
Hans Poppe: Kabisa, kwa sasa unaona tuna viungo watano, washambuliaji watano. Hivyo tuko vizuri na hii itaongeza ushindani na ubora kwao.

SALEHJEMBE: Timu yenu imekuwa ikionekana haifanyi vizuri katika mechi za mwisho za ligi, hili mmelifanyia kazi katika usajili wenu?
Hans Poppe: Kulikuwa na matatizo ya kimfumo na ndiyo yalikuwa tatizo katika hili.

SALEHJEMBE: Matatizo ya kimfumo yapi?
Hans Poppe: Hili suala la kutojitegemea, mfano wachezaji kusajiliwa na watu binafsi. Mwisho wengine wanaanza kucheza chini ya kiwango au kuonyesha utovu wa nidhamu kama madai sijui hawajalipwa mshahara. Ukata pia unachangia mwendo wa timu kutokuwa mzuri, lazima tukubali hili. Imetuathiri sana.

SALEHJEMBE: Sasa hilo mmelifanyiaje kazi?
Hans Poppe: Tayari tumepata ridhaa ya wanachama kubadili mfumo, watu wakiingia na kuwekeza, hivyo ni fedha na tutaitumia kuendesha timu kwa ushindani.


SALEHJEMBE: Mliwahi kulalamika kwamba kuna wachezaji wanawahujumu, hili mlilikumbuka?
Hans Poppe: Ikishakuwa lenu moja, rahisi sana kuthibiti mambo. Mwanzo mambo hayakuwa pamoja, Friends of Simba wengine walikaa kando. Lakini sasa wengi wamerudi kwa nguvu moja kama unavyojua kauli mbiu ya Simba. Imetusaidia kusajili vizuri na tunaamini tutaenda vizuri.

SALEHJEMBE: Simba ilikuwa na sifa ya kukuza vijana katika kikosi chake. Safari hii, Simba inaonekana imeamua kuachana kabisa na vijana?
Hans Poppe: Tuna vijana watano katika kikosi chetu, tumewapandisha. Tumechukua wachezaji wazoefu, lazima tukubali vijana nao wanahitaji muda ili kufikia kiwango sahihi.


SALEHJEMBE: Si vibaya tukisema mmechoshwa na vijana?
Hans Poppe: Labda ni wazi, hatuna muda huo tena, tumekaa miaka minne bila ubingwa. Miaka mingine miwili ya kuwakuza hatuna. Ndiyo maana tumelenga wachezaji wazoefu kwa lengo la kwenda sawa na ushindani. Wengine vijana tunawapeleka kwa mkopo, baadaye warejee na kuendelea kuitumikia Simba.

SALEHJEMBE: Aliyekuwa nahodha wenu, Hassan Isihaka vipi, naye mmeona hajakomaa?
Hans Poppe: Kwa ripoti ya mwisho ya kocha inaonekana alikuwa anasumbuliwa na uzoefu, alikuwa na papara sana na wakati mwingine alitoa nafasi kwa wapinzani kushambulia zaidi kwetu. Akicheza timu nyingine, basi itamsaidia kupata uzoefu na siku moja atarejea Simba.


SALEHJEMBE: Mmempeleka kwa mkopo timu gani?
Hans Poppe: Kweli sina uhakika sana lakini nakumbuka tulizungumza na African Lyon.

SALEHJEMBE: Katika usajili wenu wa sasa, mna Laudit Mavugo na Vital’O nao wamewasilisha jina lake katika Shirikisho la Soka la Burundi kama sehemu ya usajili wao, hamkumalizana nao?
Hans Poppe: Mavugo si mchezaji wa Vital’O, ni mchezaji wa timu inaitwa Solidarity na Vital’O walimsajili kwa miaka miwili kwa mkopo.

SALEHJEMBE: Mnalihakikishaje hilo, mnawaamini vipi hao Solidarity?
Hans Poppe: Tumefika hadi kwenye shirikisho lao, tumehakikisha kwamba Solidarity ndio wenye mchezaji.

SALEHJEMBE: Mmemalizana na Solidarity?
Hans Poppe: Tuko kwenye mazungumzo ya mwisho.

SALEHJEMBE: Kama mpo kwenye mazungumzo, Mavugo ameonekana kwenye picha akisaini mbele ya rais wenu, Evans Aveva, hii ni sahihi, kumsainisha kabla ya kumalizana?
Hans Poppe: Ngoja nikufafanulie, kila kitu kipo vizuri. Mjadala ni kwamba, tumsajili moja kwa moja au nasi tumchukue kwa mkopo kutoka Solidarity kama walivyofanya Vital’O.

SALEHJEMBE: Vipi kuhusiana na suala la Uwanja wa Bunju maana wewe ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa Uwanja!
Hans Poppe: Kuanzia leo (juzi), tunaamini baada ya mwezi mmoja, Simba itaanza kufanya mazoezi kwenye uwanja wake.

SALEHJEMBE: Tumesikia aliyefanya kazi ya Uwanja wa Azam Complex, ndiye mnamleta kumalizia kazi yenu?
Hans Poppe: Hadi sasa tuna kama asilimia 60 hivi, kazi inaendelea na mtaalamu kutoka China ambaye kweli alishiriki kazi ya Azam Complex atakuja kutandika kapeti.

SALEHJEMBE: Atatandika kapeti kwa siku ngapi?
Hans Poppe: Unajua hata mimi nilijua unatandika tu, lakini kuna aina ya mambo mengi ya kitaalamu, ‘leya’ kadhaa za mchanga na kadhalika. Halafu yatapitishwa mabomba na baada ya hapo, ndiyo kutandika kapeti.

SALEHJEMBE: Kapeti linawasili lini?
Hans Poppe: Tayari lipo bandarini, limeshawasili. Na likitolewa basi mara moja kazi ya kulisuka wakati wa kuweka itafanyika.


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV