August 8, 2016


Kiungo wa Simba, Shiza Kichuya aliyetokea Mtibwa Sugar, ameanza kuwadatisha mashabiki wa klabu hiyo wa jijini Dar kutokana na uwezo mkubwa anaoonyesha mazoezini lakini mwenyewe amempigia saluti kocha wake, Joseph Omog akidai mazoezi yake si ya kitoto na watakuwa fiti zaidi msimu ujao.

Simba tangu ilipotoka kambini Morogoro imekuwa ikifanya mazoezi kwenye Viwanja vya Boko Veterani na mashabiki wamekuwa wakifurika kutazama maujuzi ya mastaa wao wapya. Juzi Jumamosi jioni, licha ya wengi kumpokea kwa mbwembwe straika Laudit Mavugo, wengi wao walijikuta wakiduwazwa na uwezo uliokuwa ukionyeshwa na Kichuya.  

Simba itavaana na AFC Leopards ya Kenya, leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki siku ya Simba Day ikiwa ni pamoja na kutambulisha wachezaji wapya.

Kichuya alifunguka kuwa, Omog amekuwa hataki mchezo kufuatia mazoezi anayoyatoa ikiwa ni pamoja na kuwaandaa ipasavyo washambuliaji kuhakikisha wanafanya kile anachokihitaji.

“Mazoezi kwa jumla ya mwalimu yapo vizuri kwani kila mchezaji ameonekana kumuelewa ipasavyo kocha kwani kwa asilimia kubwa amekuwa akiwaandaa washambuliaji kuhakikisha wanakuwa vyema kuelekea mchezo wetu wa Simba day.


“Lengo letu ni kuhakikisha tunafanya vyema kuelekea mechi hiyo kwa ushirikiano wa pamoja kwani kila mchezaji ana shauku ya kuweza kushinda,” alisema Kichuya.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV