August 8, 2016



Na Saleh Ally
AZAM FC ni kati ya timu zilizofanikiwa kubeba ubingwa zikiwa na umri mdogo sana. Inawezekana hazikuwa zimemaliza hata shule ya msingi.

Hata kama haina wanachama lakini inajivunia mengi na hasa suala la maendeleo, ndiyo inayomiliki miundombinu bora kwa ajili ya soka, ikiwezekana kuliko timu zote kongwe za Afrika Mashariki.

Azam FC haina mashabiki wengi sana, lakini wachache walioipenda, lazima watakuwa wamevutiwa na mwenendo bora wa mpangilio wa maendeleo.

Yanga na Simba, ndizo zinazoongoza kwa mashabiki wengi zaidi ikiwezekana Afrika Mashariki na Kati. Lakini zina ugonjwa mkubwa unaohusiana na neno maendeleo. Hazina na huenda si jambo la hivi karibuni.

 Wazee walioanzisha Yanga mwaka 1935 na Simba 1936, walikwenda wanabadilika hadi kuziwezesha timu hizo kumiliki majengo katikati ya Jiji la Dar es Salaam. Lakini sasa ni zaidi ya miaka 40 tokea zimekuwa na majengo kwa mara ya kwanza, hakuna jingine jipya.

Mohammed Dewji ametangaza kuwekeza Simba, akitaka kupata hisa asilimia 51 ili amwage Sh bilioni 20. Tayari ametangaza kutoa nafasi kwa kipindi cha mpito na ameuomba uongozi kufanya kwa miezi mitatu, hii ikiwa ni baada ya mabadiliko kupitishwa na wanachama.

 Lakini kinachoendelea sasa ni wanachama au mashabiki wa Simba na wale wa wapinzani wao kuendelea kulumbana na wanachoangalia ni bei ya uuzwaji wa klabu yao kama ni sawa au si sawa.

Ukweli wa faida, hakuna anayejadili kwa kuwa kwa zaidi ya miaka 75, Simba na Yanga zimeendelea kujivunia ubingwa pekee lakini si vinginevyo.

Inawezekana kabisa yako masuala ya msingi ya kujadili hasa faida kwa kuwa suala la umiliki wa mtu mmoja au kampuni lipo tena wazi kama ambavyo tumeona England na kwingineko.

Lakini kikubwa ambacho kinapaswa kujadiliwa ni suala la faida zake ni zipi, klabu itapata nini, wapi mipaka, upi ni mwisho wa kuhoji na kadhalika.

Nafikiri mjadala kama huu ambao unahusisha kipindi cha mabadiliko ya mpira nchini haupaswi kumalizwa kishabiki na watu kujadili kuwa “mmenunuliwa” au “mmekodiwa” huku vicheko vikifuatia.

Huu ni wakati wa utulivu, Wanasimba kwa kuwa wamepitisha, basi watoe nafasi kwa uongozi wao na kama kuna kamati nayo ipewe ifanye kazi yake kwa usahihi.

Kama nilivyowahi kueleza, litakuwa jambo la msingi kupitisha jambo baada ya kugusa kila sehemu husika badala ya haraka. Ninaamini miezi mitatu aliyoomba Mo, inatosha kwa Simba kufanya hivyo.

Miezi hiyo mitatu itatosha kama utaratibu utakwenda na watu wanaofanya mambo yao kitaalamu au kwa kuhoji lakini si kugeuza ni mambo ya kawaida au malumbano ya furahisha genge. Ukiwa na chuki na Mo, basi hutaki mabadiliko, ukiwa unafurahishwa naye sana, basi mabadiliko yapite hata bila kuhoji. Haiwezi kuwa sahihi.

Kuzuia mabadiliko haya ambayo yameanza kujitokeza ni kujidanganya. Asilimia kubwa kisoka duniani ambako kuna maendeleo makubwa, masuala ya hisa au umilikishaji kwa matajiri upo na mafanikio yanaonekana. Inawezekana bado kuna sehemu kama Hispania kama Real Madrid na Barcelona, wanatumia wanachama na wanafanikiwa.

Lakini hapa Tanzania, tumetumia wanachama kwa zaidi ya miaka 80, wote mnajua tumefeli. Hivyo wawekezaji, wakiwa na sapoti ya wanachama au mashabiki, basi wanaweza kuleta mabadiliko.

Kweli soka ni ushindi na ndiyo furaha yenyewe, lakini dunia imebadilika. Sasa ni ushindi na maendeleo na hayo hayapatikani kwa “kuuza” maneno kwenye vijiwe pekee, badala yake kubungua bongo na kufanya matendo yanayolenga kuleta maendeleo.

Dunia inapaa kwa kasi ya kimondo, lazima tukubali kwamba tumeachwa sana, tena siku nyingi. Hivyo tuangalie, suala hili na lilipofikia, si ushabiki wa uwanjani ni uhai wa klabu yenu na uhai wa mapenzi ya mioyo yenu, msiiache ikafa nyie mikitaniana.




0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic