August 17, 2016


Ishu ya mchakato wa kubadili mfumo wa uongozi wa Simba SC bado ipo kwenye majadiliano na juzi usiku kulikuwa na mkutano baina ya mfanyabiashara, Mohammed Dewji na Kamati ya Utendaji ya Simba kwa ajili ya suala hilo.

Hiyo imekuja baada ya Dewji maarufu kama MO kutoa mapendekezo yake juu ya kununua hisa asilimia 51 kwa thamani ya bilioni 20. Suala hilo limeonekana kuungwa mkono na wanachama na mashabiki wengi wa klabu hiyo.

Mmoja kati ya watendaji wa timu hiyo ameliambia Championi Jumatano kuwa mkutano huo ulihusu zaidi kusikiliza mapendekezo ya MO akiwa na mtaalam wake wakitoa mchanganuo namna wanavyotaka kuiongoza timu na jinsi gani itanufaika.

 “Ilikuwa ni ishu ya majadiliano kwanza kati ya kamati ya utendaji na Mo akiwa na mtaalamu wake, kwamba klabu iende vipi baada ya mfumo wa hisa kuingia, inanufaikaje na mambo mengine kama hayo kisha kamati ya utendaji nayo izungumze kwa wanachokiona kabla ya kuingia makubaliano,” alisema mtoa taarifa huyo.

Hata hivyo, alipotafutwa Makamu wa Rais wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ kuzungumzia hilo, alieleleza kuwa kwa sasa asingependa kuzungumzia kwa kuwa lina mambo mengi na linahitaji utulivu na kila kitu kikishakamilika basi wataweka kila kitu wazi.


“Bado mchakato unaendelea na ni suala linalohitaji mchanganuo, kwa hiyo likiwa tayari tutaweka wazi Wanasimba wasiwe na wasiwasi maana hapa kuna vitu viwili vinakwenda kwa wakati mmoja, ishu ya mabadiliko na udhamini,” alisema Kaburu.

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV