August 17, 2016

Japokuwa mshambuliaji mpya wa Simba, Mrundi, Laudit Mavugo amefanikiwa kuwapagawisha mashabiki wa timu hiyo kutokana na kiwango alichokionyesha lakini benchi la ufundi la timu hiyo limesisitiza kuhitaji kumuona zaidi katika mechi za Ligi Kuu Bara kwa hesabu maalum kabla ya kuthibitisha ubora wake kwa sasa.  


Mavugo aliyetua Simba hivi karibuni akitokea Vital’O ya Burundi, tayari ameshuhudiwa na mashabiki wa timu hiyo katika mechi mbili za kirafiki dhidi ya AFC Leopards ya Kenya waliyoshinda 4-0 na URA ya Uganda waliyotoka sare ya 1-1 na wakapitisha kuwa kweli ni jembe jipya.


 
Hata hivyo, hali hiyo iko tofauti kwa kocha msaidizi wa Simba, Mganda, Jackson Mayanja aliyesikia kauli za mashabiki hao na kusisitiza kuwa si rahisi kutoa majibu ya kitaalamu kuwa Mavugo ataisaidia vipi Simba mpaka pale atakapolionyesha hilo katika mechi takribani tano za Ligi Kuu Bara msimu ujao ambazo ni sawa na dakika 450.

“Nimesikia kila mmoja akitoa alichokiona kwa Mavugo lakini ni vigumu kusema lolote kwa sasa kuhusu Mavugo, anajulikana ni mzuri lakini suala la kama atakuwa na faida kwa Simba msimu ujao ni vyema yakasubiriwa majibu ya uwanjani kwa takribani mechi tano za kwanza za ligi kuu.

“Kwangu katika mechi mbili za kirafiki ni ngumu kusema itakuwa hivi au vile kwa msimu ujao, labda kitu rahisi kinachoonekana kwa sasa katika kikosi ni mabadiliko ya wachezaji ambao kwa sasa wanapambana na ushindani umekuwa mkubwa zaidi.

“Hii ni tofauti na msimu uliopita, kwamba mtu akipata kadi au kuumia inakuwa tatizo kutafuta mbadala wake lakini kwa sasa hatuwezi kupata shida katika hilo, anayekuwa ndani mzuri na anayekaa benchi pia yupo vizuri,” alisema Mayanja mchezaji wa zamani wa KCCA ya Uganda.

 CHANZO: CHAMPIONI


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV