August 27, 2016Na Saleh Ally aliyekuwa Hispania
UNAPOWAZUNGUMZIA washambuliaji wawili wa Lionel Messi na Cristiano Ronaldo nje ya miji ya Barcelona na Real Madrid, mambo yanakuwa tofauti kabisa na inavyokuwa ndani ya miji hiyo.

Wote wawili, wanatoka nje ya nchi ya Hispania ambao wanavutiwa sana kuwaunga mkono vijana kutoka katika maeneo yao.

Lakini kutokana na nguvu ya Messi na Ronaldo, Wahispania wanawachukulia ni kama wazaliwa wa nchini humo.
Ronaldo anatokea nchi ya jirani ya Ureno, Messi anatokea Argentina, mbali. Lakini amefika Hispania akiwa na miaka 13, hivyo anaonekana ni kama yuko nyumbani na maisha yanaendelea vizuri.

Nguvu ya wachezaji hao katika miji hiyo na hata mingine ni kubwa sana ingawa pia ina tofauti kubwa katika mambo kadhaa.


Barcelona na Messi:
Gazeti la Championi, lilifanya ziara katika miji yote miwili na kufanya mahojiano na mashabiki na wakazi mbalimbali kuhusiana na wachezaji hao.

Unapokuwa katika Jiji la Barcelona, asilimia kubwa ya wanaovaa jezi za Barcelona, naweza kusema ni kwa asilimia 90 zinakuwa na jina la Lionel Messi mgongoni.

Umaarufu wa Messi uko juu sana licha ya kwamba kuna magwiji wengine wa Klabu ya Barcelona kama Xavi Hernandez na Iniesta ambao wanaheshimika hata katika miji mingine ya Hispania.

Messi anaonekana ni shujaa namba moja wa Barcelona kwa kipindi hiki. Kila mmoja anamkubali na kama utataka kuonekana ni mwendawazimu au kupata kipigo katika sehemu ambazo zina masela wengi basi onyesha unampinga Messi.


Watu wana hamu ya kumuona Messi kuliko Barcelona yenyewe. Umaarufu wake ni uwanjani na nje ya uwanja. Lakini hata eneo analoishi la Pedralbes lina ulinzi mkali.
Utaona licha ya ujio wa Neymar na Luis Suarez ambao wanafanya vizuri. Katika Jiji la Barcelona, hakuna aliyefikia nusu ya heshima yake kama shujaa wa klabu na mji.

Kama nilivyowahi kuandika, kwamba watu wanaamini anachangia kuleta watalii wengi, anawaingizia fedha kuanzia wale wenye mahoteli hadi madereva taxi. Wachuuzi wa biashara ndogondogo, bado wanaamini, Messi ni sawa na sumaku ya kuwavuta watu kutoka sehemu mbalimbali.


 Madrid na Ronaldo:
Heshima ya Ronaldo ipo juu katika Jiji la Madrid ambalo ni kubwa kuliko yote nchini Hispania na ndiyo makao makuu ya nchi hiyo.

Kwa vijana, hauwezi kuwaeleza lolote kuhusiana na Ronaldo ambao wenyewe wanamuita kwa jina la The Beast, yaani Mnyama.

Lakini Ronaldo anakumbana na upinzani mkubwa sana kutoka kwa mastaa wengine kwa kuwa pale Madrid, Atletico Madrid na yenyewe ina nguvu yake. Hauwezi kufananisha na Barcelona ambayo inatamba pekee na Espanyol iliyo katika mji huo inaonekana haina nguvu sana.

Kuna Fernando Torres ambaye ni mtoto wa nyumbani. Lakini utaona kuna wengine kama Koke, ambao wana heshima ya juu.

Hawa wanakuwa na nguvu kwa kuwa wanatokea upinzani si kama ilivyo kwa Messi, Iniesta na Xavi ambao wote wanatokea Barcelona.

Hivyo heshima ya Ronaldo, inakutana na upinzani kwa vijana na mashabiki wa Atletico Madrid ambao hawawezi kukubali hata kidogo kumshangilia.

Lakini bado anaendelea kuwa na nguvu kama ile ya Messi, kwamba wengi wanaokwenda pale. Wangependa kumuona yeye au kwenda kutembelea Uwanja wa Santiago Bernabeu unaomilikiwa na Madrid lakini kila mmoja angependa kuona picha ya Ronaldo.


Mwisho inabaki hivi; wote wawili ni mtaji mkubwa wa kuingiza fedha kwa klabu hizo kupitia biashara ya kila siku bila ya kujali zinacheza au la.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV