August 8, 2016



Na Saleh Ally
MABINGWA wa England, Leicester City ni timu ya familia moja nchini Thailand.

Familia hiyo inajulikana kwa jina la Srivaddhanaprabha, imeiongoza Leicester City hadi kutwaa ubingwa. Leo kuna Watanzania wanataka kuingia na kushangilia na kinachowavutia ni mafanikio, hakuna kingine.

Chelsea kabla ya kumilikiwa na Roman Abramovich, huenda kulikuwa na Watanzania wawili au watatu. Leo kuna maelfu kwa kuwa imefanya vizuri mfululizo.

Manchester City pia, ilionekana kibonde na isiyo na mashabiki lakini leo hadi hapa nyumbani ina mashabiki chini ya umiliki wa Mansour Bin Zayed Al Nahyan, anayeimiliki kwa asilimia 87 na Serikali ya China asilimia 13. Hadi serikali ya taifa la pili kwa uchumi duniani, linamiliki timu ya ligi kuu.

Hakuna timu inayoshiriki Ligi Kuu England isiyo na mmiliki kwa maana ya kampuni au mtu.

 Ujerumani, wameweka asilimia 51 kwa wanachama na 49 kwa wamiliki wengine binafsi. Nao wana mafanikio yao hata kama ni timu chache kama Bayern Munich na Borussia Dortmund.  

Hispania hali kadhalika, timu kubwa zaidi za Real Madrid na Barcelona ni mali ya wanachama lakini bado uendeshaji unaongozwa na bodi na anayechaguliwa kuwa rais wa klabu sharti awe na uhakika kimaandishi angalau uwezo wa kukopa benki kiasi kisichopungua euro milioni 50 (zaidi ya Sh bilioni 120), ili apate dhamana hiyo, lazima awe milionea. Jiulize, wanachama vipi wanataka milionea awe kiongozi wao wa juu kabisa?

Wanajua faida ya milionea kwa kuwa lazima atakuwa ni mfanyabiashara aliyepitia mengi na anajua njia za kupita. Ndiyo maana hawakusema mwanachama yeyote tu mwenye kadi.

Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji ambaye kila mmoja wetu anajua ni  bilionea, ameamua kuwekeza Yanga ikiwa ni siku chache tu baada ya bilionea mwingine, Mohamed Dewji ‘Mo’ kuamua kununua hisa asilimia 51 za Simba.

Kumekuwa na mijadala mingi sana, hasa mitandaoni. Wengi wakiwananga wanachama wa Yanga kwa uamuzi wao wa kupitisha Manji kuwekeza kwa miaka 10. Wengi wao wanaonekana kuwa mashabiki zaidi kuliko hoja za msingi, mfano ni ule ujumbe unaoelezwa kuwa wa Tundu Lissu anayeshangaa timu kukodishwa kama roli, nafikiri hili suala ni ‘siriaz’, vema kuweka utani kando.

Wako wanaotoa mfano wa Hispania, bila kueleza kilichofanyika hadi kufikia hapo. Mashabiki wa Madrid dunia nzima ni zaidi ya milioni 40, lakini ina wanachama 91,000 tu ambao hulipa ada hadi euro 123 (293,831) kila mmoja kwa mwaka.

 Yanga ina mashabiki zaidi ya milioni 20 hapa nchini, wanachama wake hawafiki hata 100,000. Wameamua kupitisha klabu yao kwa Manji awekeze kwa miaka 10 na faida ya asilimia 75 itakwenda kwake, 25 kwao. Kukiwa na hasara yote inabaki kwake na umiliki wa majengo na viwanja unaendelea kubaki kwa wao wanachama. Hapa hasara ni ipi?

Nani anataka kusema Yanga ilijiendesha kwa faida na wanachama walifaidika nayo, mwaka gani? Nani anayesema kumuacha Manji awekeze kwa miaka 10 ni hasara kwao? Kivipi wakati wameimiliki kwa miaka 81 na karibu yote imekuwa ni hasara na inafaidisha wajanja wachache hasa viongozi waliokuwa na nia ya kushibisha matumbo yao tu!

Makampuni makubwa yapo, wanahofia kuingia sababu ya migogoro na hofu ya kuchafuliwa jina na wanaojiita wamiliki lakini kiuhalisia wanakuwa hawachangii lolote kimaendeleo hasa linapofikia suala la kulipa fedha, mfano ile ya ada.

Utaona nimefafanua England, ni umiliki hadi asilimia mia wa makampuni au familia. Ujerumani karibia nusu kwa nusu, Hispania ni asilimia mia wanachama na mfumo wa bodi.

Lakini Tanzania tayari tumefeli na mfumo wa wanachama, hakuna anayeweza kupinga hili labda ni mgeni katika mpira. Hii ni uthibitisho tunatakiwa kuhama na kujaribu mfumo mwingine.

Kupitisha kwa Wanayanga Manji awekeze kwa miaka 10, hakuna dhambi kama wamefeli kwa miaka rundo. Siku anairudisha timu yao, uhakika kutakuwa na mabadiliko kwa maana ya miundombinu na ikiwezekana mfumo kifedha.

Neno kukodisha, lisitumike vibaya na kuwakatisha tamaa wanachama wa Yanga ingawa ni vizuri katika masuala ya uingiaji mikataba ndiyo wanapaswa kujua mifumo na mipaka katika uwekezaji huo.

Miaka kumi, Manji amekwama wanachukua timu yao, nembo yao na kuendelea na hamsini zao. Lakini watakuwa wamejifunza jambo.

Kila siku wapenda soka nchini wameigeuza TP Mazembe ya DR Congo kuwa mfano. Wanajua ina mashabiki na wanachama lakini inamilikiwa na mfanyabiashara Moise Katumbi. Dunia imebadilika na hakuna anayeweza kuyazuia mabadiko hayo kwa mikono.

Kikubwa ni kuangalia kabla ya kuingia kipi kifanyike. Tuache mihemko na ushabiki maandazi kwenye masuala muhimu, badala yake tujadili hoja na nini cha kufanya ili kuyavaa mabadiliko hayo. Tumekaa kwenye kisiwa peke yetu, miaka nenda rudi ndiyo maana mafanikio kwetu ni bahati nasibu.


Kama Leicester wangehofia kuiunga mkono timu ya familia, leo isingebeba ubingwa na wote tumeona baada ya ubingwa walioingia mitaani na kukesha wakisherehekea ni mashabiki na si familia ya Srivaddhanaprabha.

4 COMMENTS:

  1. hii blog ni miongoni mwa blog ninazozipenda sana kutokana na uandishi wenye weledisio ile blog ya mtu anajiita binti nani sijuii..

    ReplyDelete
  2. KAKA UKO SAWA SANA, KUNA BAADHI YA BLOG MMILIKE WAKE ANAINGIZA USHABIKI WAKE NA SIASA NDANI YAKE.....HALAFU HUYO LISU SIASA NA SOKA WAPI NA WAPI BHANA?

    ReplyDelete
  3. teh teh teh.....lakini si imekodishwa kama daladala?

    ReplyDelete
  4. Kwa mara nyengine tena nakupongeza sana kwa kalamu yako nzuri ambayo humfanya kila msomaji wako kufurahia jamboambalo unalielezea ukiondoa mbali ushabiki,kimsingi ni ukweli usiopingika kwamba soka sasa liko zaidi kibiashara bila ya kuwa na nguzo imara za uchumi huwezi kuendesha soka katika ulimwengu huu pia kwa nchi kama ya tanzania ilivyo chamaa cha soka hakina msaada wowote zaidi ya kuziumiza klabu ambazo ziko chini yake kwa kuzinyonya kwa kuchukua mapato makubwa kwa kila mechi bila ya kuzisaidia kwa jambo lolote lile ili kuvimbisha matumbo yao,kwa maana hiyo uamuzi wa Yanga kumpa timu Manji mimi nakubaliana nao na hata wa Simba kumpa timu Dewji naunga mkono ikumbukwe msimu uliopita Simba walishindwa hata kulipa wachezaji mishahara yao kwa kweli hilo halipendezi nadhani wakiwa na Dewji hilo halitotokea tena na wale viongozi ambao wanajinufaisha binafsi itakuwa ndio mwisho wao wanachama na wapenzi wa vilabu hivyo viwili ni lazima wakae chini na watafakari kwa kina sio wajaribu kupinga bila ya kuwa na hoja za msingi.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic