August 1, 2016



Na Saleh Ally
 KATIKA mkutano wa wanachama wa Simba uliofanyika jana jijini Dar es Salaam, wanachama wa klabu hiyo kongwe walionekana wanataka mabadiliko na wamelenga kuona mwanachama mwenzao Mohammed Dewji anapewa jukumu la kuisongesha Simba mbele.

Dewji maarufu kama Mo, alishatangaza ofa ya Sh bilioni 20 ili amilikishwe asilimia 51 ya hisa za klabu hiyo na baada ya hapo, mapambano ya ‘Nguvu Moja’ yasonge mbele.

 Baada ya kauli hiyo ya Mo Dewji, mashabiki wa Simba wamekuwa na hamu kubwa kuona anakabidhiwa timu mara moja, naye aingize fedha zake na baada ya hapo, aanze kupambana kuhakikisha kila kitu kinakwenda vizuri.

Wanachama waliokuwa kwenye mkutano wa Simba jana, walipiga kelele kutaka kuona uongozi unajadili ajenda ya tisa iliyokuwa ikihusisha mabadiliko. Hii iliendelea kuonyesha kwamba wanachama wa Simba wanataka mabadiliko. Utaona hata Simba ilipofunga bao katika mechi ya kirafiki dhidi ya Moro Kids Ijumaa iliyopita, mashabiki walishangilia wakimtaja Mo Dewji.

Naelewa mashabiki wa Simba ni wavumilivu sana, lakini inaonekana wamechoka kwa kuwa wanataka furaha ndani ya mioyo yao na hakuna anayeweza kupinga kwamba mwendo wa wapinzani wao Yanga na sasa Azam FC umeifanya Simba kuwa timu namba tatu ya Tanzania.

Hili limetokea kwa miaka minne, miwili ikiwa chini ya Ismail Aden Rage na miwili chini ya Evans Aveva. Hawa Simba wamechoka ndiyo maana wanaona hakuna zaidi ya mabadiliko ili waweze kupambana.

Uongozi wa Simba katika mkutano wa jana, ulimaliza kwa kusema kwamba umekubaliana na suala la kwenda kwenye mabadiliko na mchakato unaanza.

Mchakati hauwezi kuwa wa wiki moja, vizuri wanachama wangeelewa maana niliona wengi wakishangilia lakini hakukuwa na maswali waliyouliza ili kupata ufafanuzi kuwa mchakato huo unaweza kuwa ni wa muda gani.

Kama hiyo haitoshi, bado wanachama hao wanapaswa kupewa somo kuwa kuhama kutoka kwenye uendeshaji wa klabu kwenda kwenye kampuni si jambo la siku moja kwa kuwa linajumuisha mambo mengi kama kubadili katiba, masuala ya uendeshaji na kadhalika.

Baada ya kuingia kwenye kampuni ambako kutakuwa na hisa ambazo ndizo Mo Dewji anataka hizo asilimia 51, bado kutatakiwa kutolewa somo ambalo wanachama wa klabu hiyo pamoja na mashabiki wanapaswa kulijua na uendeshaji wake, faida na hasara zake ziko vipi.

Kipindi cha mabadiliko hakiwezi kuwa kifupi na kipindi hicho hakiwezi kwenda kama upepo wa kimbunga kwa kuwa mambo yanahitaji kufuata taratibu na hatua.

Hofu yangu ni moja tu, kwamba wakati Simba wanakwenda katika kipindi cha mabadiliko, wanachama na uongozi wasijikute wameingia kwenye kundi la kujichanganya na kuanza kuipa klabu yao wakati mgumu.

Wanaweza kuingia huko kwa kuwa kila mwanachama ana hamu ya kuingia kwa pupa. Hii inaweza kupoteza maana ya Simba kufanya maandalizi mazuri kwa ajili ya msimu ujao na haitakuwa na faida tena kwao zaidi ya hasara maradufu.

Kwa kuwa uongozi umekubali, basi vizuri uonyeshe kweli kwamba unalishughulikia hilo suala na hatua zinapigwa ili Mo kama anaingia kwa kile ambacho wanaamini ni sahihi, basi kila kitu kiwe wazi.

Lakini Mo Dewji kwa kuwa ni Mwanasimba na ushiriki wake katika maendeleo hauna hofu hata kidogo kwa kuwa mwaka 2003 alionyesha mfano ambao Simba hawajaurudia tena tokea wakati huo walipoing’oa Zamalek katika michuano ya klabu bingwa Afrika na kuivua ubingwa ikiwa ni klabu bora Afrika, basi aingie na kushirikiana na viongozi.

Kama viongozi wa Simba na Mo Dewji watashirikiana sasa, itakuwa ni rahisi sana hata kwenda kwenye mabadiliko wakiwa pamoja na hii itaisaidia Simba kutoyumba hata kidogo wakati inabadili mambo na mwisho iwe mfano kwa wengine wakiwemo wapinzani wao wakubwa na watani Yanga.



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic