Na Saleh Ally
UNAPOMZUNGUMZIA Zlatan Ibrahimovic, kama ingekuwa hapa nyumbani Tanzania, kwa lugha nzuri ungeweza kumuita mtoto wa ‘uswahilini’.
Kijana ambaye amekulia maisha duni kabisa kwa kuwa familia yake ilitengana mapema na baba yake akaamua kuishi maisha ya upweke peke yake, huku Zlatan akibaki kuishi kwa mama yake ambaye alikuwa akiuza hadi madawa ya kulevya.
Eneo la Rosengard nchini Sweden, ndilo alilozaliwa Zlatan. Ni eneo wanaloishi watu wa maisha ya chini kabisa na asilimia kubwa ni wakimbizi. Hata watu wazawa wa Sweden wanaliona ni kama eneo la hovyo kabisa.
Zlatan amekua akitafuta heshima na kwa waliobahatika kusoma kitabu kinachohusu maisha yake ambacho simulizi yake huandikwa kila Jumamosi kwenye Gazeti la Championi, amekuwa akieleza namna ambavyo amekuwa akikwepa kuendelea kudharauliwa kwa kuwa ndiyo maumivu makubwa ya moyo wake.
Akiwa mdogo, dharau ndicho kitu alichokutana nacho kila siku kwa kuwa familia yake ilikuwa duni, waliishi kwenye nyumba mbaya, walikula chakula duni, walikuwa na runinga ya hali ya chini na kila kitu kwao kilikuwa duni.
Zlatan alipambana kupata mafanikio kwa kuwa hakutaka kudharauliwa tena kwenye soka kwa kuwa siku ya kwanza kuanza kucheza kwenye viwanja vya watoto wa Rosengard, alionekana ni mwembamba kama Fidodido (jina alilobandikwa) mwenye pua kubwa ambaye huenda angeangushwa hata na nguvu ya mpira kama angepokea pasi. Kwa kifupi, mafanikio ya Zlatan ni kuhakikisha anaikataa dharau.
Kukataa dharau imekuwa ni chachu ya mafanikio ya watoto wengi wa masikini, mfano mwingine ni Bondia Floyd Mayweather ambaye ilifikia hatua yeye na wenzake wakalala hadi watu nane katika chumba kimoja.
Sasa Zlatan ni mshindi wa karibu kila kitu katika ngazi ya klabu. Binafsi ameshinda rundo la tuzo akiwa karibu na kila timu kubwa katika kila nchi na kila ligi.
Zlatan alianza na ubingwa wa Sweden, Uholanzi akiwa na Ajax, baadaye Italia ambako amezichezea Juventus, Inter Milan, AC Milan halafu Barcelona akiwa Hispania na baadaye akahamia Ufaransa ambako ilionekana kama amekosea lakini ni mchezaji aliyeisaidia PSG kurudi kwenye ramani ya soka duniani kwa mara nyingine.
Sasa ametua England, ambako anakwenda kucheza Manchester United iliyoyumba na kupoteza matumaini. England na Ujerumani ndiyo sehemu pekee ambazo hajaonyesha alichonacho katika ligi zote kubwa za Ulaya. Lakini bado yuko kwenye kampeni ya kukataa dharau.
Huenda changamoto ya dharau ya Kocha Arsene Wenger wa Arsenal ambaye alimkataa Zlatan mwanzoni kabisa, inaweza kumfanya apambane kuhakikisha anabeba kombe akiwa na Man United, tena safari hii akiwa ameungana na mpinzani mwingine mkubwa wa Wenger, Jose Mourinho.
Mourinho na Zlatan ni timu ya makombe, licha ya kila mmoja kufanya peke yake lakini wote wamewahi kushinda pamoja ubingwa wa Serie A ya Italia, pia wakabeba ubingwa wa Ulaya dhidi ya Barcelona ya Hispania. Sasa wametua pamoja Man United, wanataka tena ubingwa au mafanikio.
Wakati wa kupambana kupata mafanikio, hakuna ubishi Zlatan ndiye baba mpya mwenye nyumba katika kikosi cha Man United kwa kuwa aliyekuwa mkuu wa mashambulizi, Wayne Rooney tayari alionekana amepoteza mwelekeo. Hakuwa tishio tena wala kiongozi ambaye angetangulizwa mbele kuwatisha wapinzani.
Zlatan anaanza kuwatisha hadi wachezaji wenzake, kwamba unapokuwa naye katika kikosi kimoja lazima ujitume kwa kuwa si mtu anayetaka mchezo na hiki anacho Mourinho.
Lakini kama hiyo haitoshi, Mourinho naye ni mtu wa mwendo au mfumo wa aina hiyo, hivyo vijana walio Man United akiwemo nahodha Rooney wanajua kabisa wanacheza na watu wenye njaa ya makombe ambao hawataki kutanguliza utani hata kidogo.
Ushindi kwao si swali la kuuliza, lakini kupambana ndiyo maisha ya kila siku kwa kuwa Zlatan ameonyesha kila alipopita, hakuna timu aliyocheza bila kubeba kombe na Mourinho pia amefanya hivyo. Sasa kwa nini washindwe wakiwa na Man United?
Presha ya kupambana ambayo wanayo Zlatan na Mourinho, inawavaa wachezaji na benchi zima la ufundi la Man United, kwamba ni lazima wafanye kazi kweli, hakuna utoto wala utani kwa kuwa mbele yao kuna Simba wenye njaa na wanataka kupambana kupata ushindi.
Zlatan ametwaa makombe na mafanikio makubwa katika ligi kubwa tofauti zaidi ya Rooney. Hakuna alipokwenda akashindwa, hivyo hata Rooney atalazimika kuungana na kufuata ari ya mwenye nyumba mpya ambaye rafiki yake mkubwa ni makombe.
0 COMMENTS:
Post a Comment