September 9, 2016

Kutokana na kushindwa kutumia nafasi za kufunga anazopata mara nyingi, mshambuliaji wa Simba, Mrundi, Laudit Mavugo, sasa atalazimika kukubali kupata somo maalumu juu ya nafasi yake hiyo kutoka kwa mtu mwingine zaidi ya makocha wake wawili, Joseph Omog na Jackson Mayanja.

Mavugo

  Jukumu hilo la kumnoa Mavugo kutokana na tabia ya kukosa nafasi nyingi za wazi, limekabidhiwa kwa meneja wa Simba na aliyekuwa mshambuliaji wa timu hiyo, Mussa Mgosi ambaye amejipa kazi hiyo.

Licha ya kuwa amefunga mabao mawili dhidi ya Ndanda FC na Ruvu Shooting katika Ligi Kuu Bara msimu huu, bado amekuwa na kasoro ya kukosa nafasi za wazi, jambo ambalo linaonekana kutowafurahisha Wanasimba.


Mgosi (kulia) enzi zake alipokuwa akiichezea Simba


   Mgosi aliyewahi kucheza soka la kulipwa katika timu ya DC Motema Pembe ya DR Congo ameliambia Championi Ijumaa kuwa, amejipa majukumu hayo ya kumfundisha Mavugo mbinu bora za kufunga kutokana na kuona straika huyo ana upungufu kadhaa.

“Nimemuona Mavugo kwa namna anavyocheza pamoja na upungufu wake ambapo sasa nimeamua kujipa majukumu ya kumuweka chini na kumfundisha namna ya kucheka na nyavu zaidi kuliko hivi anavyofunga sasa.

“Ni mchezaji mzuri lakini anakosa umakini wa vitu kadhaa ambavyo nikimpiga ‘msasa’ basi atakuwa moto wa kuotea mbali, idadi ya mabao pamoja na umakini wake wa kucheka na nyavu utakuwa mkubwa kuliko huu wa sasa alionao,” alisema Mgosi ambaye jezi yake namba 11 inavaliwa na Mavugo.



SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic