September 10, 2016Yule beki wa Simba ambaye hajacheza hata mechi moja ya Ligi Kuu Bara, Besala Bukungu mazoezini ni mbishi na sasa ana staili mpya kwani ukimpiga chenga tu anakuchania jezi.

Katika mazoezi ya jana Ijumaa jioni kwenye Uwanja wa Boko Beach Veterani, Bukungu raia wa DR Congo alimchania straika wa timu hiyo, Laudit Mavugo ‘bib’ maarufu kama bipsi au kizibao alichokuwa amevaa.

Bukungu alimchania bipsi Mavugo baada ya kumvuta pindi alipomuacha kitu kilichowachekesha mashabiki walioudhuria mazoezi hayo.

Beki huyo wa kulia ambaye jana katika mazoezi hayo alicheza kama beki wa kati, pia alimchania mara mbili Shiza Kichuya bips yake baada ya kumpiga chenga. Ibrahim Ajib naye alichaniwa bips yake mara moja.

Bukungu hakucheza mechi za nyuma baada ya hati yake ya uhamisho wa kimataifa (ITC) kuchelewa kufika nchini. Hata hivyo, imeelezwa kuwa ITC imeshafika. Kutokana na hali hiyo, Bukungu kesho anaweza kuwemo kwenye kikosi cha Simba kitakachocheza na Mtibwa Sugar mechi ya Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam saa 10:00 jioni.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV