September 10, 2016

Baada ya kutofungwa hata bao moja, Kipa wa Ndanda FC, Jeremiah Kisubi, amesema hajafungwa na straika Donald Ngoma wala Obrey Chirwa wa Yanga kwani anawajua udhaifu wao.

Ndanda Jumatano wiki hii iliamua kumuweka benchi kipa wake Jackson Chove na nafasi yake akacheza Kisubi ambaye hakuruhusu bao hata moja na kuiwezesha timu yake kupata suluhu dhidi ya Yanga.

Katika mchezo huo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Ngoma raia wa Zimbabwe na Chirwa raia wa Zambia, walijitahidi kufunga lakini hawakufanikiwa.

Wakati Yanga ikilalamika haikupata bao kutokana na ubovu wa sehemu ya kuchezea ya uwanja huo, Kisubi yeye alisema: “Nilijua uchezaji wa Ngoma na Chirwa, hivyo sikuruhusu wanifunge kirahisi.
 


“Licha ya kugundua mbinu zao, lakini nao hawakuwa makini katika kazi yao na mara zote walicheza kama wana uhakika kuwa watapata bao dakika zijazo hicho ndicho kilichowaponza.

“Sasa uchezaji ule wa Ngoma na Chirwa naamini nikiongeza mazoezi hawataweza kunifunga hata siku moja endapo nikipata nafasi ya kucheza tena dhidi yao timu zetu zikikutana.”

Kisubi ana historia ya kuokoa penalti ya Ngoma katika mchezo wa ligi kuu msimu uliopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambapo walitoka sare ya mabao 2-2.


SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV