September 19, 2016

Na Saleh Ally, Barcelona
Katika makala iliyopita ya mahojiano kati ya Championi na beki wa zamani wa Barcelona, Eric Abidal, alieleza namna alivyofanikiwa kurejea uwanjani na kucheza.

Hata hivyo, kulikuwa na taarifa kwamba Abidal alikuwa mwoga sana kucheza kwa hofu huenda alikuwa bado hajapona vizuri ugonjwa wa ini ambao ulimdhoofisha.

Huku tukiendelea na mahojiano, tuliendelea kubaki ofisini kwake kwa muda mrefu, takribani saa mbili, hata baada ya mahojiano.

Abidal ambaye sasa ni Mwislamu, maneno mengi amekuwa akitanguliza neno “Inshallah” kuonyesha kinachofuata ni majaaliwa ya Mwenyezi Mungu.

Beki huyo ni mcheshi, pia ana uwezo mzuri wa kuzungumza lugha za Kifaransa, Kihispania pia Kiingereza ambazo angalau unaweza kumuelewa vizuri.

“Kucheza haikuwa kitu kigumu, ila hofu ilikuwepo kiasi kama binadamu. Kuumwa si kitu kizuri, kunaogopesha lakini kwa kuwa nilishapata maandalizi kwa siku nyingi, sikuwa na hofu sana.
“Nilianza kucheza kwa tahadhari kama sehemu ya kuusikiliza mwili wangu kama uko vizuri. Lakini baadaye nilizoea na kuanza kucheza kama zamani,” anasema.

Abidal alianza maisha yake ya soka katika klabu ndogo ya Lton Duchere iliyopo nchini Ufaransa, baadaye akajiunga na Monaco B na baada ya mechi nane tu akapandishwa timu kubwa ya Monaco ya Ufaransa pia.

Baadaye aling’ara akiwa na Lille aliyoichezea mechi 62 kuanzia mwaka 2002 hadi 2004, hadi alipojiunga na Lyon pia ya Ufaransa ambayo alidumu kuanzia mwaka 2004 hadi 2007 akiwa amecheza mechi 76, akasajiliwa na Barcelona.


Katika maisha yake ya soka, Barcelona ndiyo timu aliyoichezea mechi nyingi zaidi kwenye soka la kulipwa. Aliitumikia kwenye mechi 125 na ndiyo maana anaona yupo nyumbani. Alitua Barca mwaka 2007 hadi 2013 alipoondoka na kujiunga na Monaco tena, akaichezea mechi 26, akaamua kwenda Olimpiacos aliyoichezea mechi tisa tu, akaamua kustaafu tena ghafla.

Kawaida kwa mujibu wa Abidal, maisha ya wachezaji wengi wa Barcelona, hayaishi hata baada ya maisha ya soka na klabu hiyo.

 “Ukicheza Barcelona kwa zaidi ya miaka miwili, basi utaona kuwa wewe ni familia, ndiyo maana kuna klabu ya Wakongwe wa Barcelona. Hii inatukutanisha pamoja mara kwa mara.

“FC Barcelona si kwa ajili ya mpira pekee, Barcelona ni familia. Hata baada ya kustaafu, watu hubaki pamoja. Hukutana na kujadiliana mambo mbalimbali.

“Lakini wachezaji waliostaafu wana mawasiliano mazuri hata na wale wanaocheza. Klabu kupitia uongozi, inapokea ushauri au mawazo. Inashirikiana na wachezaji wake wa zamani kwa mambo mengi na inapohitajika kusaidia inafanya hivyo.

 “Unapokuwa Barcelona, basi ujue upo kwenye familia. Barcelona kama inavyoeleza kwenye nembo ya klabu yenyewe. Kweli ni zaidi ya klabu,” anasema Abidal.

 “Mfano unawaona kina Messi na wengine wanaocheza sasa. Tumekuwa tukiendelea kushirikiana kwa mambo mengi sana,” anasisitiza.

 “Mfano wakati wa hili jaribio la mapinduzi linalotokea nchini Uturuki, tulikuwa jijini Istanbul kwa kuwa kuna mechi ya wakongwe ilikuwa imeandaliwa na aliyeiandaa ni Samuel Eto’o.


“Messi alikuwa ni sehemu ya waalikwa. Hivyo yeye na wachezaji wengine walikuwa wanakuja kuungana nasi. Wakati tukiwa hotelini, kukaibuka taarifa za mapinduzi ya nchi.

“Awali tuliambiwa nchi imepinduliwa, hofu ilitawala na kukawa na maneno mengi yasiyo na uhakika. Baadaye tulipata taarifa kwamba jeshi la serikali lilikuwa limezima mapinduzi hayo.

 “Hata hivyo, tayari amani ilishatoweka, kusingekuwa tena na mechi. Tukaweka msisitizo ni lazima turejee nyumbani. Mara moja kilichofanyika ni kukodi ndege, safari ya kurejea Barcelona ikaanza mara moja.

 “Tunamshukuru Mungu, wote kwa pamoja tulifika salama tukiwa na ndege ya kukodi. Lakini ilikuwa hofu barabarani wakati tukienda uwanja wa ndege,” anasema.





 



 Abidal anaamini maisha yake katika Jiji la Barcelona yanakuwa ni sehemu sahihi. Angependa kuendelea kuishi hapo kwa kuwa yuko karibu na familia yake.

 Kuhusiana na kustaafu kwake ghafla mwaka jana akiwa na Olimpiacos, Abdal anasema aliona wakati mwafaka umefika na hakupaswa kuhesabu namba, mfano kuona mechi tisa ni chache, huenda angecheza hadi zifike 20.

Sasa amewekeza nguvu zake kwenye taasisi yake inayojulikana kwa jina la Abidal22 Foundation, ambayo inaendelea kusaidia watoto mbalimbali wenye matatizo ya afya dunia nzima.

 Mfano anaangalia kama mambo yakienda vizuri, anataka kuanza kuelekeza misaada katika nchi za Afrika akianzia na Kusini mwa Bara la Afrika huku akieleza wazi kwamba siku moja, angetamani kufika Tanzania.
“Hakika ningetamani sana siku moja kufika Tanzania. Nimepata sifa zake, watu wake na mambo mengi. Inshallah, ninaamini siku moja nitakuja,” anasema Abidal.

MWISHO

BAADA ya makala hii, usikose makala nyingine tamu ya mahojiano ya ana kwa ana yaliyofanywa na Gazeti la Championi katika Chuo cha Soka cha Barcelona maarufu kama La Masia jiji Barcelona. Makala ni kati ya gazeti hili na beki Gerard Pique wa Barcelona ambaye aliwahi kuichezea Manchester United na sasa ni mme wa mwanamuziki maarufu, Shakira.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic