September 7, 2016


Na Saleh Ally
UGANDA imefuzu kucheza michuano ya Kombe la Mataifa Afrika maarufu kama Afcon ambayo safari hii inafanyika nchini Gabon, mwakani.

Michuano hiyo ni migumu, ni madini na aghalabu kwa nchi za Afrika Mashariki kushiriki. Si rahisi kusikia Tanzania, Kenya au Uganda zimepata nafasi. Hata zile za Burundi au Rwanda.

Badala yake, Sudan au DR Congo na mara chache Ethiopia angalau zimekuwa zikijaribu kuchungulia kwa kuvuka mpaka na kuingia kwenye michuano hiyo ambayo wenyewe ni Afrika ya Magharibi na Kaskazini, angalau pia Kusini mwa Afrika.

Mara ya mwisho, Tanzania ilishiriki mwaka 1980 wakati Uganda mara ya mwisho ilikuwa 1978.

Katika michuano iliyopita kuwania kucheza michuano hiyo, Uganda waliteleza katika mechi ya mwisho. Lakini walikuwa ndiyo timu ambayo walionyesha kuwa na nafasi kuliko nyingine za ukanda wetu.


Wakati wanafuzu safari hii, wanachukua nafasi hiyo wakivuka kutoka katika kundi lenye timu kama Botswana na Burkina Faso, pia Comoro ambao waliwafunga bao 1-0 katika mechi ya mwisho, wakafuzu.

Uganda wanafuzu huku wakiwa na mambo mengi sana ambayo yanaonyesha kwamba sisi tunatakiwa kuwa juu kabisa kimaendeleo zaidi yao.

Ligi Kuu ya Uganda, udhamini wake hauko juu kama ule wa Tanzania kwa kuwa una makampuni mengi zaidi. Kama utazungumzia ushindani, utaona timu za Tanzania, nyingi ni imara zaidi.

Unapozungumzia ushiriki wa michuano iliyo chini ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf), timu zetu zimekuwa angalau zikifanya vizuri kama utalinganisha na Uganda. Mfano mzuri kwa kipindi cha miaka minne, Yanga na Azam FC wamefanya vizuri zaidi, hauwezi kulinganisha na zile za Uganda ambazo karibu kila moja ilitolewa awali.

Uganda wana ligi ambayo hakuna wachezaji wa kulipwa, pia malipo ya wachezaji katika ligi hiyo yako chini kabisa. Kamwe hauwezi ukalinganisha hata nusu na yale wanayopata wachezaji wa nyumbani au wa kigeni wanaocheza Ligi Kuu Bara.

Muonekano kwa maana ya jezi zinazotumika Ligi Kuu Tanzania Bara, zina kiwango cha juu na hii inaonekana Watanzania tumekuwa na mafanikio katika mambo ambayo hayana matunda kama ambavyo Uganda wamepiga hatua.

Hakuna sehemu kusipokuwa na majungu, lakini Tanzania yamezidi na kikubwa kinachoiendesha Tanzania kufeli ni ubinafsi ambao unatokea moyoni na Watanzania wengi hasa viongozi wa klabu, vyama na mashirikisho wamekuwa wakipambana kuzipata nafasi za kuongoza kwa ajili ya maslahi yao binafsi na si maendeleo ya soka ya Watanzania.

Ukiangalia viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa sasa nguvu zimeelekezwa katika maandalizi ya uchaguzi ujao, namna gani wataweza kupita na inawezekana ni rahisi sana kumsaidia ambaye atakuwa tayari kuwasaidia siku itakapofikia.

Hisia za mioyo yao zimejaa ubinafsi, mioyo ya wengi walio katika mpira ni wavivu wa kuamini Tanzania inataka mabadiliko. Kila anayeimba kubadilika, anamaanisha anataka kubadilika yeye na familia yake au kabila lake na wala si Tanzania au Watanzania.

Kwa maana ya mwenendo kisoka, wachezaji walioisaidia Uganda zaidi ni wale wanaocheza nje ya nchi hiyo. Uganda hawana wachezaji England, Hispania au kwenye ligi kubwa. Lakini ligi za nchi za Ulaya Mashariki, Asia na kwingineko Afrika.

Hao wamerejea nyumbani na nguvu na mawazo tofauti na wanajifunza nje na kupeleka wanachojifunza nyumbani.

Wachezaji wa Tanzania, kila anayekwenda kucheza nje, miezi sita mingi, anataka kurejea tena nyumbani kwa kuwa makuzi yetu hayaendani na kokote duniani. Maana wachezaji wamezoea kushangiliwa, kuonekana wafalme hata kwa kiwango kidogo.


Mwisho unaona wenye makuzi tofauti, mfano Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu, hawakucheza nchini muda mrefu na mwisho wakajifunza tabia za hovyo za waliojifunza wengine ambao wanashindwa kubaki kucheza nje na kujifunza ili matunda wayalete nyumbani na kutusaidia. Wabinafsi, ndiyo maana wanashindwa kubaki nje ya Tanzania kwa kuwa kule, ushindani unaanzia nje ya uwanja na tabia au nidhamu ni jambo namba moja.


Viongozi na wachezaji, hili la Uganda msilifumbie macho. Fumbueni mlione, acheni masikio yenu wazi msikie na mwisho niwakumbushe, mara ya mwisho Uganda, nusura wafuzu wakiwa chini ya kocha ambaye alikuwa hapa nyumbani akaonekana ni wa kawaida tu, huyu ni Sredojevic Milutin ‘Micho’. Sasa wamefuzu wakiwa na huyohuyo.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic