September 7, 2016


Huku zikiwa ni raundi tatu zimechezwa tangu msimu mpya wa Ligi Kuu Bara uanze, mshambuliaji wa Azam FC, Rafael Bocco, amefanikiwa kujiwekea rekodi tatu ikiwa ni pamoja na kufunga bao la mapema na bao la dakika za lala salama pamoja na kuongoza katika ufungaji.

Straika huyo wa Azam FC ambaye ndiye tegemeo kwa sasa kufuatia kuondoka kwa aliyekuwa mshambuliaji wa timu hiyo, Kipre Tchetche, amesaidia katika ushindi wa mechi mbili walizocheza licha ya kuwa katika nafasi ya tano ya msimamo wa ligi kwa kuwa na pointi nne.

Mechi ambazo Bocco ametupia ni ile dhidi ya African Lyon katika dakika ya 93, ambapo amefunga kwenye dakika za nyongeza ikiwa hakuna mchezaji yeyote aliyefunga katika dakika hizo na kwenye mchezo dhidi ya Majimaji uliopigwa kwenye Uwanja wa Chamazi, alifanikiwa kufunga mabao mawili moja likiwa ndani ya dakika ya pili, ambalo ndilo bao pekee lililofungwa mapema zaidi katika raundi hizo tatu na lingine amefunga dakika ya 83.

Mabao mengine yaliyofungwa katika dakika za mapema hadi sasa ni lile la Shija Mkina ambalo amefunga dakika ya tano katika mchezo kati ya Mtibwa Sugar na Ndanda FC matokeo yakiwa 2-1, huku lingine likiwa la Hassan Mwasapile la dakika hiyohiyo ya tano kati ya Toto African na Mbeya City ambao walitoka 1-0.

Aidha, mabao mengine yaliyofungwa katika dakika za  lala salama katika raundi hizo tatu ni pamoja na lililofungwa dakika ya 92 na Juma Mahadhi wa Yanga katika ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya African Lyon, huku bao lingine likifungwa na Raphael Daudi wa Mbeya City dakika ya 89 katika ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Mbao FC.

Bocco ndiye mchezaji anayeongoza katika kufumania nyavu kwa sasa kutokana na kufunga mabao matatu huku akifuatiwa na Rashid Mandawa wa Mtibwa na Raphael Daudi wa Mbeya City, wote wamefunga mabao mawili kila mmoja.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic