September 12, 2016

Juuko Murshid, juzi jioni alitua Bongo kwa ajili ya kuanza kuitumikia Simba lakini kauli aliyoitoa Rais wa Simba, Evans Aveva hivi karibuni, moja kwa moja inamfanya kocha wa kikosi hicho, Joseph Omog kumpa nafasi ya kucheza kikosini kwake beki huyo mahiri raia wa Uganda.

Murshid aliipa presha kubwa Simba, kwani tangu aende kuitumikia timu ya taifa ya Uganda, wiki moja iliyopita hakurejea hadi juzi huku siku zake zikiwa hazipatikani. Ilielezwa kwamba amefanya mgomo baridi kutokana na kukerwa kuwekwa benchi na kocha Joseph Omog. Tayari ameambiwa aandike barua ya kujieleza.

Lakini Aveva amesema anataka kuona wachezaji wote wa kimataifa waliopo ndani ya Simba wanapata nafasi ya kucheza kwani ni moja ya makubaliano yao na benchi hilo la ufundi linaloongozwa na Omog.


Tangu msimu huu uanze, Juuko amekosa nafasi ya kucheza kikosini hapo huku nafasi anayoicheza ya beki wa kati ikichezwa na Method Mwanjali na Novaty Lufunga.

Ikumbukwe msimu uliopita, Juuko alitengeneza ukuta imara kikosini hapo kiasi kwamba alikuwa ndiyo tegemeo na alipokosekana basi Simba ilikuwa na wakati mgumu, lakini msimu huu imekuwa tofauti.

Taarifa za uhakika kutoka ndani ya benchi la ufundi la timu hiyo, zinasema Aveva amekuwa akishangaa kuona Juuko hajapewa nafasi mpaka sasa wakati anaamini uwezo bado anao wa kuitumikia Simba kama ilivyokuwa msimu uliopita.


“Unajua hakuna anayeamini kama Juuko sasa hivi hana nafasi kikosini, hata rais Aveva naye anashangaa hilo wakati awali walikubaliana na Omog na kumhakikishia kwamba profesheno wote lazima awape nafasi, lakini utaona mpaka sasa kama vile dalili hizo hakuna.


“Wakati wa kipindi cha usajili Omog aliambiwa achague wachezaji ambao anaona watakuwa msaada kikosini isije kutokea kama huko nyuma kujaza wachezaji halafu hawana nafasi, kwani hatutaki kuona tunarudi kule tulipotoka. Kitendo cha Juuko kuwekwa benchi kinamshangaza Aveva na sasa anataka aone akichezeshwa,” alisema mtu huyo.


Hivi karibuni, Omog alisema Juuko bado ana nafasi ya kucheza kikosini hapo na kwa sasa anampumzisha mpaka pale ligi itakapochanganya kwani aina ya uchezaji wa Juuko ni wa nguvu, hivyo anamuandaa kuja kupambana na timu ngumu ambazo ndiyo levo ya beki huyo.

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV