September 12, 2016

Kama washambuliaji wa Azam FC, John Bocco na Mrundi, Laudit Mavugo wa Simba walidhani Amissi Tambwe wa Yanga ndiyo basi tena baada ya kutofunga kwenye mechi mbili za awali, walikosea kwa kuwa tayari mshambuliaji huyo ametupia mbili fasta kwenye mechi ya wikiendi iliyopita kisha amewaachia ujumbe.

Tambwe hakufunga bao kwenye mechi mbili za awali za Ligi Kuu Bara kabla ya kufunga mabao mawili kwenye mechi yao ya tatu dhidi ya Majimaji, wikiendi iliyopita waliyoshinda kwa mabao 3-0 na kumfikia Mavugo mwenye mabao mawili huku akimkaribia Bocco aliyefunga mara tatu.


Tambwe

Mavugo

Tambwe, raia wa Burundi, ameeleza kwamba anafahamu kuwa washambuliaji wenzake hao pia wana nia ya kuchukua kiatu cha ufungaji bora msimu huu, hivyo anaamini mapambana yatakuwa makubwa lakini hatakata tamaa na atapambana mpaka tone la mwisho.


“Ni kweli sikufunga kwenye mechi za awali na hiyo ni kawaida tu, wala hakuna tamaa, wakati mwingine unaweza kucheza mechi hata tano na usifunge lakini nashukuru nimeanza kufunga na naona ushindani ni mkubwa, kila mtu anataka kuwa mfungaji bora.


“Nitahakikisha napambana nao (Bocco na Mavugo), maana nao ushindani wanauweza na wote tupo kwenye chalenji moja, tunapokea changamoto ya aina moja,” alisema Tambwe, mfungaji bora wa msimu uliopita.


Msimu uliopita, Tambwe alitwaa kiatu hicho akiwa na mabao 21, akimuacha mpinzani wake aliyefunga mabao 19, Hamis Kiiza aliyekuwa akiichezea Simba. Nyuma ya msimu huo, Tambwe alimaliza kwenye nafasi ya pili akiwa na mabao 14 nyuma ya Simon Msuva wa Yanga aliyefunga mara 17.


Kabla ya hapo, katika msimu wa kwanza wa Tambwe kukanyaga Ligi Kuu Bara, msimu wa 2013/14 alifanikiwa pia kutwaa kiatu hicho baada ya kutupia jumla ya mabao 19.  

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV