September 16, 2016

WAZIRI NAPE

Na Saleh Ally
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo, Nape Nnauye ameanza kuonyesha kwamba anataka kufanya mabadiliko katika mambo mbalimbali katika michezo.

Tumemshuhudia akijitokeza katika sehemu mbalimbali katika masuala ya michezo tena bila ya kujali ni aina gani ya michezo na amekuwa akionyesha wazi kwamba anataka mabadiliko.

Tukubali kwamba Nape ameanza vizuri kwa kuwa amekuwa msemakweli, kwenye upungufu anasema, kwenye kitu kizuri anasema. Michezo imekuwa ikihitaji mtu wa namna hiyo kwa muda mrefu sana.

Hivi karibuni alijitokeza tena kwenye Uwanja Uhuru na kusikiliza malalamiko ya mashabiki ambao yalimfikia kwamba vyoo na mambo kadhaa yanayohusu usafi, yalikuwa na walakini.

Kiongozi bora ni yule anayesikiliza matatizo ya watu wake na kuyafanyia kazi. Nape ameonyesha mfano na vema akaungwa mkono kwa kuwa ameonyesha ni tofauti na wengine waliopita ambao zaidi ungewasikia kama wageni wa heshima na si kujihusisha na matatizo moja kwa moja.

Pamoja na yote, Nape alifanya uzinduzi wa tiketi za elektroniki baada ya kupitia mambo kadhaa na baadaye kufanikiwa kuhakikisha utengenezaji wa mitambo na baadaye kuizindua kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Tunajua jambo hilo la tiketi za elektroniki limeshindikana kabisa, lilianza katika mechi chache tu, mambo yakaenda kombo. Ikaonekana kuna walakini kupindukia, jambo ambalo baadaye lilielezwa kuna baadhi ya watu walikuwa wanataka kukwamisha kwa makusudi.

Waliotaka kuona kila kitu kinafeli, walifanya kila  juhudi ili mambo yaende vibaya. Halafu ionekane imeshindikana ili waendeleze mazoea yao na maisha yao ya kuiba fedha za mpirani.

Wote tunajua, wanaoongoza kuiba fedha za mpirani ni viongozi wa mpira. Viongozi wa mpira ndiyo wanaofaidika na fedha za pembeni za mpirani.

Tunajua viongozi wa soka wanauza tiketi feki, wana mipango yao mibaya ambayo inawafaidisha wao na kuudhoofisha mpira wa Tanzania kwa kuwa unawafaidisha wachache ambao wanalia kwenye vyombo vya habari kwamba wanausaidia mpira kumbe ndiyo wanaoumaliza kwa faida au maisha yao wenyewe.

Watu hao wasingependa mabadiliko hata kidogo, wasingependa kuona alichokianzisha Nape kinafanya kazi kwa kuwa ni sawa na kuwaondolea riziki na walivyozoea kubata fedha kwa ulaini au kwa mteremko.

Viongozi wa soka wamefanya kila linalowezekana kujitengenezea njia ya kupata fedha haramu ndani ya mchezo wa soka. Huku wakilia kinafiki kwenye hadhira kuonekana wao ni watetezi namba moja wa mchezo wa soka, jambo ambalo ni uongo, uzandiki na ubabaishaji mkubwa na wa hali ya juu kabisa.

Angalizo kwa serikali na Waziri Nape, kuanzisha tiketi za elektroniki ni sawa na kuanzisha vita. Kwa kuwa wengi wanaoizunguka michezo kamwe hawatafurahia na inawezekana walikuwepo siku ya uzinduzi na hawakupenda, lakini walitabasamu wakionyesha wako pamoja naye.

Waziri Nape anapaswa kujua waliomzunguka wengi wana ngozi ya kondoo na mara nyingi wanamchekea kutaka kuonyesha wako pamoja naye, lakini kwa kuwa anaoiondoa riziki, hakika hawawezi kumfurahia.

Hivyo haitakuwa rahisi na wako  watafurahia kuona anafeli na mwisho ionekane suala hilo haliwezekani kabisa. Mwisho mambo yarudi kama zamani na wao mkono uendelee kwenda kinywani kwa njia ya mkato.

Mimi niwaase, kwamba wameiba muda mrefu, wameiba vya kutosha huenda sasa ni wakati mzuri wa kuamua mawili, kukubali mabadiliko au kushika jembe warudi kijijini wakalime kama watakuwa wanataka mchekea.

Sasa wayapishe mabadiliko na klabu na wachezaji wafaidike kweli. Hata wanaotoa fedha, pamoja na kufurahia lakini wayaone mabadiliko.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV