September 16, 2016

Na Saleh Ally, Barcelona
Kama ambavyo niliwahi kukuelezea kuhusiana na namna ambavyo Uwanja wa Cam Nou mali ya Barcelona unavyoingiza fedha nyingi hata kama timu hiyo inakuwa haichezi.

Uwanja huo ni kitega uchumi hasa, ni maarufu sana kuliko watu wengi maarufu duniani. Watu husafiri kutoka sehemu mbalimbali duniani kwa lengo la kuutembelea.


Nikishuhudia Tuzo ya FIFA Ballon d'Or
Kanisa la Camp Nou
 Kwa wapenda michezo na hasa soka, uwanja huo una mambo mengi sana kwao na hasa historia na rekodi ambazo zimewekwa ndani ya uwanja huo, kila mmoja angependa kufika na kujionea mwenyewe na si kuhadithiwa au kusoma kwenye mitandao.
 
Kumbuka, Camp Nou ndiyo uwanja mkubwa zaidi wa soka duniani katika viwanja vya klabu au vinavyojulikana katika mchezo wa soka.

Kama utazungumzia duniani, basi kuna Uwanja wa Taifa wa Korea Kaskazini, wenyewe ndiyo mkubwa zaidi kwa maana ya kuingiza idadi kubwa zaidi ya watazamaji.

Ukiwa ndani ya uwanja huo, unapata nafasi ya kupitia kwenye makumbusho ya klabu hiyo. Utaona makombe mbalimbali ambayo Barcelona imewahi kuyatwaa. Kwa rekodi, ndiyo klabu iliyoshinda makombe mengi zaidi kwa yale yanayotambulika.

Kuna mengi ya kuona, mfano mechi mbalimbali za klabu hiyo zilizopita timu hiyo mafanikio makubwa. Zinaonekana na utapata nafasi ya kuangalia.

Watu hupita kila sehemu, chumba cha waandishi wa habari kwa ajili ya mikutano, vyumba vya kubadilishia nguo na kadhalika.

Utaona Barcelona nao ni watu waliojipanga hasa. Kwamba kila kitu kilikuwa na kipo kwenye mpangilio na wanaingiza fedha nyingi kwa siku.

Josep Iola, mmoja wa maofisa wanaoshughulikia ziara za ndani ya uwanja huo, anaamini Barcelona ndiyo klabu inayotembelewa na watu wengi zaidi.
 
“Hapa ndiyo tuko busy kuliko klabu nyingine yoyote duniani. Utaona namna watu walivyo na wasivyopungua na wakati Barcelona imetwaa La Liga au ubingwa wa Ulaya, huwa kazi ngumu sana hapa.

“Wakati mwingine klabu hulazimika kukodi wafanyakazi wa muda kutokana na waliopo ambao ni zaidi ya 150 kuzidiwa,” anasema alipozungumza na Championi.

Kilichonivutia zaidi au kunishangaza, ni kanisa lililo ndani ya uwanja huo. Si kubwa sana, lakini vipi kuna kanisa na linaendeshwa vipi?
 

  
Si kubwa, lina mabenchi kama nane tu ya kukalia wakati wa ibada na unaweza kushangazwa kuona likiwa katika mpangilio mzuri sana.

Wachezaji wa Barcelona hupata nafasi ya kusali kabla na baada ya mechi ndani ya kanisa hilo ambalo liko ndani ya Uwanja wa Camp Nou.

Raha zaidi, kanisa hilo lipo kwenye eneo la njia ya kwenda uwanjani. Maana yake wachezaji lazima wataliona wakati wa kwenda au kurejea. Hivyo ni chaguo la kila mmoja kuchagua.

Wachezaji kwa pamoja au kila mmoja anapoona ana nafasi ya kuingia humo, huingia na kusali kila kabla ya mechi inayofuatia.

Wachezaji wamekuwa wakihakikisha wanafanya hivyo kwa kuwa ni utamaduni wa Barcelona, miaka nenda rudi na suala la kusali na kumuomba au kumshukuru Mungu linapewa kipaumbele.

Iola anasema, ni nadra sana kwa mchezaji kupita bila ya kusali, mara chache wachezaji wenye imani ya dini kama Uislamu, wao hufanya ibada nje ya kanisa hilo. Mfano kwenye vyumba vya kubadilishia nguo au sehemu nyingine.


    
“Unajua kila klabu ina utamaduni wake, hili kanisa ni sehemu ya utamaduni, lakini halimzuii mtu kuabudu anavyotaka kwa kuwa hata wachezaji Wakristo hawalazimishwi kama mtu hajisikii kuabudu hapo,” anasema.

Wakati fulani, watu waliruhusiwa kufunga ndoa katika kanisa hilo dogo, lakini baadaye ikawa idadi na msululu mkubwa ambao baadaye ulisababisha usumbufu.

Mwisho, klabu hiyo ikazuia na sasa kutaka litumike na wachezaji pekee badala ya watu wakiwemo wa nje ambao walipewa nafasi hapo awali.

Wachezaji wa Barcelona, hasa wale wasiopenda sana kuchanganyika na watu, hufanya ibada yao kila Jumapili kwenye kabisa hilo, safari hii wakiwa na familia zao.
 

Ndani ya Camp Nou

Sehemu ya wachezaji wanapopita kuingilia kwenye pitch ndani ya Camp Nou.

Hata hivyo, kabla ya kwenda Jumapili, hulazimika kutoa nafasi na kuelezea kama watakwenda ili maandalizi yafanyike kabla ya wao kwenda.

Kanisa na Camp Nou ni dogo, lakini ni moja ya makanisa makongwe kwa kuwa limekuwepo tokea mwanzoni mwa miaka ya 1900 hasa baada ya klabu hiyo kupata uwanja wake huo.

Pamoja na ubora, Barcelona wameonyesha kumuamini Mwenyezi Mungu ni jambo namba moja. Hivyo unaweza kujipima na kutafakari katika hilo.

Swali, vipi hakuna msikiti, wameeleza utamaduni wa klabu na nchi ya Hispania. Huenda kwa klabu nyingi hasa za Afrika, zinaweza kuweka kanisa na msikiti.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV