October 14, 2016Muda mfupi baada ya straika wa Yanga, Mzambia, Obrey Chirwa kufunga bao lake la kwanza tangu atue nchini kuichezea timu hiyo, tayari kumekuwa na maoni juu ya bao hilo.

Awali, alitegemewa kuibeba Yanga na kuwa pacha mzuri wa Donald Ngoma katika ufungaji lakini haikuwa hivyo, hivyo bao lake la juzi katika mechi dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Uhuru ndipo akafanikiwa kufunga bao kwa mara ya kwanza katika ushindi wa mabao 3-1.

Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Salum Mayanga, amesema uzembe wa mabeki wake wa kati ndiyo ulisababisha Chirwa akapata bao hilo.

“Hatukuwa makini kwenye safu ya ulinzi na tulifanya makosa ambayo mwishowe tukajikuta tukiadhibiwa kwa kuwaruhusu wapinzani wetu watufunge mabao mepesi utaona hata lile la Chirwa ni uzembe tu wa kutookoa mpira kwa wakati ndiyo ukasababisha yote yale,” alisema Mayanga. 

Bao hilo la Chirwa limekuja ikiwa ni baada ya siku 117 tangu ajiunge na timu hiyo akitokea FC Platinum ya Zimbabwe, ikielezwa kuwa alisajiliwa kwa mkataba wa miaka miwili kwa shilingi milioni 200.

Kuhusu bao la Chirwa, kocha wake mkuu Hans Pluijm alisema: “Ni jambo la kufurahia wote kuona mchezaji ambaye hakufunga kwa muda mrefu akifunga bao lake la kwanza tangu ajiunge nasi, hii itamfanya kujiamini zaidi na naamini mechi zijazo ataendelea kufunga.


“Tulipokuwa tunajiandaa na mchezo huu, mazoezini alifanya mambo adimu ambayo moja kwa moja yalinishawishi kumuanzisha kwenye kikosi cha kwanza, na kweli kile alichokifanya mazoezini kimekuja kuzaa matunda kwenye mechi.” 

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV