October 14, 2016Kiungo mshambuliaji wa Simba ambaye yupo katika kiwango cha juu kwa sasa ndani ya kikosi chake hicho, Shiza Kichuya, nyota yake imeendelea kung'ara baada ya mashabiki wa jijini hapa kuonyesha kumkubali na kumpa shangwe za nguvu katika mchezo wa timu yake dhidi ya Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine. 

Kichuya ambaye amekuwa na kawaida ya kupiga saluti mara baada ya kufunga, alipata shangwe za nguvu baada ya kufunga bao la pili kwa Simba kisha mashabiki hao kumpigia saluti kwa ishara ya kukubali kile alichokifanya. 

Mbali na hapo, mara baada ya kuumia kipindi cha pili na kulazimika kutolewa nje akiwa amebebwa kwenye machela, mashabiki wengi wa Simba walisimama na kumpigia saluti ikiwa ni ishara ya kukubali mchango wake.

Mbali na hapo, mashabiki wengi wamekuwa wakitamba mitaani na hata katika mchezo huo kuwa Kichuya ambaye alitua Simba akitokea Mtibwa Sugar mwanzoni mwa msimu huu, ndiye staa wao mpya na wanaamini atachangia kuwapa ubingwa wa Ligi Kuu Bara walioukosa kwa misimu minne mfululizo.

Aidha, akizungumzia kiwango cha timu yake, Kocha Jackson Mayanja ambaye ni msaidizi wa Kocha Mkuu wa Simba, Joseph Omog, alisema kuwa kasi waliyoanza nayo siyo nguvu ya soda na anaamini watafanya vizuri zaidi ya ilivyo sasa.

Mayanja alisema kwa sasa hawana wasiwasi na kikosi chao kutokana na kuwa na wachezaji wengi wenye uwezo mkubwa.

"Kuna watu wanadhani kasi hii itapungua, mimi niwaambie tu kuwa watasubiri sana, maana msimu huu tumejiandaa vizuri sana,” alisema Manyanja.

Kuhusu straika wao Laudit Mavugo kukaa benchi katika mchezo huo, Mayanja alisema: "Tuna wachezaji wengi hivyo hatumtegemei mchezaji mmoja, leo akicheza huyu, kesho anacheza mwingine.”


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV