October 14, 2016



Na Nkini Phillip
TAMASHA la wafungwa linatarajiwa kufanyika leo Ijumaa kuanzia saa 2 asubuhi ambapo kutakuwa na burudani mbalimbali ikiwemo kutoka kwa The African Stars ‘Twanga Pepeta’.

Burudani hiyo ambayo itakuwa na vitu vingi ikiwemo kushuhudia wanamuziki wanaotumikia kifungo cha maisha ndani ya Gereza la Ukonga, Nguza Viking ‘Babu Seya’ na mwanaye Johnson Nguza ‘Papii Kocha’ wakitoa burudani pia kutakuwa na shoo kutoka kwa msanii wa Singeli, Msaga Sumu.

Akizungumzia tamasha hilo lililoandaliwa na Kampuni ya Global Publishers, mratibu, Juma Mbizo, alisema lengo ni kuwatia moyo wafungwa na kuwaonyesha wao ni sehemu ya jamii ambapo pia mhamasishaji mashuhuri Afrika Mashariki na Kati, Eric Shigongo atakuwepo kutoa neno.

Shigongo ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Global Publishers, Wachapishaji wa Magazeti ya Ijumaa Wikienda, Uwazi, Risasi, Amani, Ijumaa na Championi, amesema anatambua wafungwa waliopo gerezani nao wanahitaji faraja na kutiwa moyo kwa namna moja au nyingine, kwani nao walikuwa na ndoto zao hivyo kuwatia moyo ni jambo jema.

“Hii si mara ya kwanza kwa Global kuandaa tamasha la namna hii, mwaka 2008 tuliandaa, tunapozungumza pamoja na ndugu zetu waliopo gerezani huwa nao wanafarijika.

“Mtu kufungwa haimaanishi kwamba hana maisha tena, haimaanishi kwamba hawezi kutimiza ndoto zake, haimaanishi kwamba alikuwa mkosaji sana asiyefaa katika jamii.

“Bado mfungwa ana nafasi ya kujitunza, kuwa na malengo, kujiandaa na kutimiza ndoto zake pindi akitoka gerezani. Mifano ninayo mingi tu, kuna wafungwa ambao  tulizungumza nao mwaka 2008, leo hii wameshatoka na wanakuja ofisini kwetu kutushukuru,” alisema Shigongo.

Kuhusu burudani nyingine kwenye tamasha hilo, Mbizo alisema kutakuwa na mbio za magunia, soka, kuvuta kamba, riadha, kula mkate na soda, kuimba na kupiga muziki.

“Itakuwa ni Nyerere Day, hivyo tutamkumbuka muasisi wa taifa hili, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kuimba, kucheza pamoja na wafungwa,” alisema Mbizo.

Aidha, Mkuu wa Gereza la Ukonga, ACP Stephen Mwaisabila, naye anatarajiwa kutoa neno katika tamasha hilo sanjari na viongozi wengine wa magereza.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic