Mshambuliaji wa Stand United, Abasrim Chidiebere anaendelea vizuri na anaweza kuanza kucheza soka katika kipindi cha mwezi mmoja.
Chidiebere aliumia baada ya kugongwa na beki wa kati wa Azam FC, Aggrey Morris, wakati timu hizo zilipokutana katika mchezo wa Ligi Kuu Bara, juzi.
Kocha Msaidizi wa Stand, Athumani Bilali ‘Bilo’, amesema Chidiebere ambaye alipoteza fahamu kwa saa sita, anaendelea vizuri na ndani ya mwezi mmoja anaweza kurejea uwanjani.
"Daktari amesema, ndani ya mwezi mmoja anaweza kuanza mazoezi. Lakini ni suala la kufuatilia afya yake kwa ukaribu kabisa," alisema.
"Kweli ameumia, taya kama mlivyoona lakini sasa anaendelea na matibabu na usimamizi ni wa karibu sana."
Chidiebere aligongwa na kusababisha apote fahamu kuanzia saa 10:20 jioni hadi 4:00 usiku.
Wachezaji wa Azam FC akiwemo Morris, walifika kwenda kumjulia hali mshambuliaji huyo aliyeanza kucheza soka nchini akiwa katika kikosi cha timu ya soka ya waandishi wa habari za michezo cha Taswa FC.
0 COMMENTS:
Post a Comment