October 14, 2016


Na Saleh Ally
HUENDA watu wengi wanaweza wakawa wamelichukulia kama utani suala la kwamba Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji amekata tamaa na alifikia uamuzi wa kuondoka zake.

Lakini katika fikra za kawaida kabisa za kibinadamu, watu lazima wajue Manji ni mwanadamu pia kama wengine na anaweza akachoshwa au kuumizwa na jambo fulani.
Suala la Kampuni ya Yanga Yetu Ltd kutaka kuikodisha timu ya Yanga na nembo ya Yanga, limekuwa gumzo na wachache wanaopinga wameonekana kuwa na nguvu zaidi.

Mfano, kwa wale wanaokumbuka wakati Manji anaanzisha suala la ukodishwaji kwenye mkutano wa dharura wa wanachama wa Yanga, alitamka wazi kwamba anawaomba aikodishe Yanga.

Hakusema ni mtu mwingine, alieleza wazi ni yeye. Waliokubali ikodishwe wanajua ni Manji na huenda walikubali kwa kuwa wanamwamini kupitia miaka nenda rudi tangu alipoweza kusaidia kupatikana kwa mwafaka wa klabu hiyo ambao uliishinda hata serikali kuutatua.
Leo utashangazwa eti kuna mjadala, kwamba Kampuni ya Yanga Yetu Ltd ni ya nani. Huyu mtu anayeibua mjadala huo, kweli alikuwa hajui au ana maslahi yake binafsi na anataka kuivuruga Yanga kwa makusudi!

Mafanikio ya Yanga kwa klabu za Tanzania yanajulikana. Hii ni klabu kongwe zaidi na imesimama vizuri na utaona misimu minne, bingwa mara tatu Ligi Kuu Bara, nafasi ya pili mara moja na mara moja ikiwa ni mara ya kwanza Kombe la FA limerejea, imelibeba.

Hakuna ubishi kulingana na mafanikio hayo, lakini hakuna ubishi kwamba Yanga inatakiwa ipige hatua kutoka hapo ilipo kwenda mbele.

Yanga imecheza robo fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho. Hakuna ubishi sasa ni nafasi ya kucheza na kufanya vizuri kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika. 

Ikishindikana, ikashuka kwenye Kombe la Shirikisho, vizuri angalau iishie nusu au kwenda fainali kabisa.
Yanga inaihitaji fedha, mtu ambaye atakuwa tayari kuwekeza fedha zake. Yanga haitakiwi kurejea nyuma tena na inawezekana kabisa kilichoikwamisha miaka mingi ni rundo la “Yanga Maslahi” kuwa wengi kuliko wale wenye lengo la kuendeleza.

Wengi wanaozuga wanaipigania Yanga katika kipindi hiki, ni wale wanaotaka kuona maslahi yao yanafanikiwa na si yale ya klabu.

Nasema wanaonyesha wana maslahi yao kwa kuwa hawana hoja za msingi hata wanapohoji. Zaidi wanatanguliza jazba au kulazimisha mvurugiko wa mambo yasiyo ndani ya hoja kwa kuwa hawana hoja ya kutetea wanachokizungumzia.

Kama Klabu ya Yanga inakwenda kukodishwa timu yake ambayo ni mzigo mkubwa, tatizo ni lipi? Wanasema utaratibu ufuatwe, lakini hawaonyeshi ukiukwaji mkubwa ambao unaweza kumzuia mtu anayetaka kuwekeza.

Nembo ya Yanga, miaka nenda rudi ipo hapo na haiingizi faida kiasi cha kusema ina faida. Timu ndiyo imebaki kuwa furaha na karaha ya mioyo ya Wanayanga.

Kipindi ambacho Yanga imekuwa kwenye utulivu wa suala la kifedha, angalau unaweza kuona mwendo mzuri, usajili wa uhakika.

Kuhoji ni haki ya kila mpenda michezo kama ninavyohoji mimi. Ni haki ya kila Mwanayanga, kama wanavyohoji hao wengine, lakini basi tuwe watenda haki na kuelekeza nguvu kwenye maisha ya Yanga yenyewe na si maslahi ya mtu mmojammoja.

Nafikiri leo itakuwa ni mara ya pili au tatu, nasisitiza, kama kuna mtu atakuwa ana chuki binafsi na Manji, huenda chini ya uongozi wake, mtu huyo alifutwa uanachama, au kuna aliyetaka kuiba alipogundulika akafutwa kazi aache kueneza sumu ya kutaka kulipa kisasi kwa ajili yake bila ya kujali maslahi ya Yanga yenyewe.

Tukubaliane, wanaotoa hoja wakijenga na kuzitoa za msingi basi hakuna ubishi kwamba hata kama upande wa Yanga Yetu Ltd kuna tatizo, basi litaweza kufanyiwa kazi na ukodishwaji ukafanyiwa aidha marekebisho au maboresho na Yanga kuweza kufanya mambo yake kwa uhakika.

Vizuri wadau mnaoanzisha hoja, zitoeni akilini lakini ujenzi wa hoja hizo uchanganywe na kwenye mioyo yenu ili ziwe zenye haki, zenye lengo la kujenga na kuisaidia klabu yenu.


Maana kama kila mmoja ataangalia nafsi yake, mfano hampendi Manji, au Yanga ikikodishwa yeye hatafaidika kamwe hamtaisaidia klabu yenu na mkumbuke, mtakuwa na deni kwa vizazi vijavyo. 

1 COMMENTS:

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic