October 10, 2016


Kicha mpya wa Toto Africans ya jijini Mwanza, Khalfan Ngassa ambaye ni baba mzazi wa mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Mrisho Ngassa, ametamba kuwa amejipanga vilivyo kuhakikisha anaiongoza timu hiyo kumaliza katika nafasi ya pili kwenye michuano ya Ligi Kuu Bara msimu huu.

Ngassa amejiunga na timu hiyo hivi karibuni akichukua mikoba ya Rogasian Kaijage ambaye alimwaga manyanga kuifundisha timu hiyo kwa shinikizo la mashabiki kufuatia matokeo mabaya.

Hata hivyo, Ijumaa iliyopita, Ngassa alifanikiwa kuianza vizuri kazi yake hiyo baada ya kiongoza Toto Africans kupata ushindi ugenini wa mabao 2-0 dhidi ya Kagera Sugar, mechi hiyo ilichezwa kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

Ngassa ambaye pia aliwahi kutumikia Simba kama mchezaji katika miaka ya 1980, alisema kuwa yale mateso ya kufungwa mara kwa mara ambayo Toto Africans ilikuwa ikiyapata sasa yamefikia tamati.

“Nawashukuru viongozi wa Toto Africans kwa kuniona na kuamua kunipatia jukumu hili na nimejipanga kuhakikisha nafanya mapinduzi makubwa kwa kushirikiana na wenzangu wote niliowakuta katika benchi la ufundi ambayo kila mpenzi wa soka jijini Mwanza atayafurahia.

“Hata hivyo, baada ya kuanza kwa ushindi dhidi ya Kagera Sugar kinachofuatia sasa ni kuhakikisha tunafanya vizuri katika mechi zetu zote zilizobakia ili tuweze kumaliza ligi hiyo katika nafasi ya pili na kama tutashindwa kuifikia, basi nafasi yetu ya mwisho iwe ya nane,” alisema Ngassa.


Toto Africans hivi sasa inashika nafasi ya 13 katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi 8 ilizozipata baada ya kushinda mechi mbili na sare mbili katika michezo nane iliyocheza mpaka sasa.

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV