October 10, 2016



Na Saleh Ally
HIVI karibuni kikosi cha timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17, Serengeti Boys kimerejea nyumbani baada ya kushindwa kufuzu kucheza Kombe la Mataifa Afrika baada ya kupoteza mchezo wao.

Walipoteza mchezo kwa kufungwa na Congo kwa bao 1-0, hivyo kufanya matokeo ya jumla kuwa 3-3 na Wakongo wakasonga mbele kwa tofauti ya bao la ugenini kwa kuwa wao walifunga mawili ugenini baada ya ushindi wa 3-2 wa Serengeti Boys jijini Dar es Salaam.

Taarifa za vijana hawa kulia baada ya mechi, hali kadhalika kocha wao, Bakari Shime kumwaga chozi, zilikuwa zinaumiza sana.


Walikuwa vijana waliopania kufika mbali, walitaka kufanya kile ambacho Watanzania wengi sana wamekuwa wakishindwa kufanya kwa kuwa maisha yetu yamezungumzwa na visingizio na uvivu tu.

Shukurani kwa Mwenyezi Mungu kuwapa nguvu ya kubadilika na kuwa tofauti, kuwa wapiganaji wa dhati ambao wameshindwa katika dakika mbili za mwisho baada ya kupigana kwa zaidi ya dakika 1000 wakipambana kupata nafasi hiyo iliyokuwa muhimu kwa maisha yao ya soka na kwa taifa letu.

Unakumbuka wakati timu hiyo ilipokuwa haifanyi vizuri, hakuna aliyekuwa akiifuatilia au kutaka kujua inafanyaje. Kadiri siku zinavyosonga mbele, mabadiliko yake wengi wakaweka imani na kuanza kuifuatilia.

Wengi waliingia na kuanza kuchangia ambalo ni jambo zuri na hata serikali ikawa karibu kuhakikisha timu hiyo inafanya vema na ikiwezekana kufika mbali.

Baada ya Serengeti Boys kukosa nafasi hiyo, imeonyesha makosa ambayo tumekuwa tukiyafanya mara nyingi katika michezo ya aina tofauti. Kwamba kuunga mkono ni kwa timu inayofanya vizuri pekee na wale walioshindwa licha ya kujitahidi, wanaonekana hawana maana.


Serengeti Boys wamerejea kimyakimya, kuna sehemu walifika na hata ule ukubwa wa mambo au idadi ya wadau ikawa inaenda inapungua na unaweza kusema kila walichofanya kiliishia baada ya mechi.

Kuna mdau mmoja ambaye ningependa kumzungumzia. Huyu alifanya kitu pekee ambacho kinaonyesha kuna mambo yanaweza kufanyika kwa ambao tunaamini ni mashujaa na kuendelea kuwapa moyo kwa ajili ya baadaye badala ya kuwakimbia mara moja na haraka baada ya kupoteza mchezo.

Tabia hii imekuwa inavunja nguvu wengi sana. Lakini mmiliki wa kampuni ya kuuza matairi na betri za magari ya Bin Slum Tyres Ltd ameonyesha njia tofauti na hili ni funzo kwa Watanzania wengine, tuamini kuunga mkono kunawezekana hata baada ya kushindwa ili kuweka nguvu ya baadaye.

Kama Serengeti Boys ingeshinda na kufuzu, kila mmoja angejitokeza kuwa karibu na kufanya mambo yaonekane kwa kiwango cha juu, huenda kwa kuwa wengi wangeamini timu ingefika hadi ikulu au kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Lakini Bin Slum waliahidi kimyakimya kwa vijana wa Serengeti Boys kama watashinda, basi wangewapa Sh milioni 3. Kama wangeshindwa basi wangeambulia Sh milioni moja tu. Hii ilikuwa ni sehemu ya kuwapa nguvu na ilifanyika moja kwa moja kwao.

Waliposhindwa, bado Bins Slum Tyres Ltd, wakafika hadi kambini mwa kikosi cha Serengeti Boys, tena hata bila ya waandishi wa habari na kuwapatia vijana hao yote Sh milioni 3 ambayo waliwaahidi kama wangeshinda.

Bin Slum Tyres Ltd wanaamini vijana hao ni washindi hata kama wamekosa nafasi ya kwenda Madagascar itakapofanyika Afcon. Lakini wanaamini kwa kuwa vijana, wana safari ndefu na walipaswa kupewa moyo na kuongezewa ari kwa kuwa safari yao kisoka ndiyo inaanza na hao ndiyo kikosi cha chini ya miaka 20, yaani Ngorongoro Hereos.

Wengine wote tuliwaacha. Sasa tujifunze kujumuika hata wakati wa majonzi na si kusubiri furaha tu. Bin Slum Tyres Ltd wangeweza kutowapa moyo vijana hao na wasingedaiwa na mtu. Basi wapongezwe kwa kuonyesha mfano na mliokubali kujifunza, basi hili liwe somo na mbadilie.




0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic