October 14, 2016


Baada ya juzi Jumatano, kufunga bao moja katika ushindi wa mabao 3-1 kwa timu yake ya Yanga dhidi ya Mtibwa Sugar, winga wa Yanga, Simon Msuva amesema hilo ni bao lake la 50 akiwa klabuni hapo na lengo lake ni kufikisha mabao 100.

Wakati akigusia kuhusu kufikisha idadi hiyo ya mabao, pia amegusia suala la yeye kuondoka Yanga na kusema kuwa ikitokea ikawa hivyo nia yake ni kwenda nje ya nchi kucheza na siyo kuhamia Simba au Azam FC ambazo ni klabu kubwa pia kwa hapa nchini.

Msuva amesema kuwa tangu aanze kuichezea Yanga miaka minne iliyopita, amekuwa akipambana kufanya vizuri na anakumbuka bao lake la kwanza alifunga msimu wa 2013/14 dhidi ya URA ya Uganda, tangu hapo safari yake imekuwa ikipanda.

“Nataka nipambane nifunge mabao mengi zaidi, ikiwezekana 100, ili siku nikiondoka Yanga, niwe na heshima, unajua haya ni maisha siwezi kuwa Yanga siku zote, ipo siku nitaondoka, lakini nataka kufunga mabao mengi na nikiondoka niwe na heshima ili siku nikirejea iwe rahisi wao kunikubali.

“Sitaki kwenda Simba wala Azam, nilizungumza na Mrisho Ngassa akaniambia yeye alifunga zaidi ya mabao 50, hiyo inanipa nguvu ya kuendelea kupambana.

“Mabao yangu hayo ni niliyofunga nikiwa Yanga pekee, nimekuwa nikiweka rekodi hiyo lakini pia kuna rafiki yangu amekuwa akinisaidia katika kuhifadhi rekodi kama hizo,” alisema Msuva ambaye msimu huu katika Ligi Kuu Bara ameshafunga mabao mawili.

Aidha, Msuva alisema anashangaa mashabiki wa timu yake kuonyesha kukosa uvumilivu pindi wanapoona mambo yamekaa vibaya na kufikia hatua ya kumzomea, amedai ameshaizoea hali hiyo na haimsumbui.

“Najua mimi ni mchezaji mzuri ndiyo maana napata matokeo mengi kutoka kwa mashabiki ninapokuwa uwanjani, kunizomea au kunipigia kelele naona ni moja ya changamoto za kunirekebisha, hii haimtokei kila mchezaji, hata Ulaya kuna baadhi wanafanyiwa hivi na ni wale ambao wanaonekana wanakosea wakati hawastahili kukosea.

“Kuna wakati itakuwa safi na watanishangilia kwa muda wote,” alisema Msuva aliyeibuka mfungaji bora msimu wa 2014/15 baada ya kutupia mabao 17.


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV