October 24, 2016


Baada ya kiungo wa Simba, Mzamiru Yassin kufanikiwa kuifungia Simba bao la ushindi katika ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mbao FC, jana akafunga tena mawili katika mchezo wao dhidi ya Toto Africans na tayari mchezaji huyo ametamba kuwa huo siyo mwisho wake na kwamba atawafunga sana msimu huu.

Kwa spidi hiyo tayari kiungo huyo ameongeza presha kwa mafowadi wa Ligi Kuu Bara baada ya kufikia idadi ya mabao manne yaliyofungwa na straika wa timu hiyo, Laudit Mavugo na mastraika wa Yanga; Donald Ngoma, Amissi Tambwe na Obrey Chirwa. 

Hata hivyo, licha ya Mzamiru kucheza mbali na goli kutokana na majukumu yake ya kiungo wa kati lakini mpaka sasa amefikisha idadi hiyo msimu huu akifunga mfululizo huku yote akiyafungia ndani ya 18.

Ukiachana na bao la Mbao alilofunga kwa kumchambua kipa akiwa ndani ya boksi, jingine la kwanza alilifunga walipocheza na Kagera Sugar kwa kuunganisha kwa kichwa kona ya Shiza Kichuya katika mechi waliyoshinda 2-0 kabla ya jana kufunga la kwanza kwa kumchambua golikipa baada ya kutengewa pasi ya mwisho na Frederic Blagnon.  

La pili alilifunga kwa shuti akiwa tena ndani ya boksi akiunga kona iliyopigwa na beki wa kulia wa timu hiyo, Janvier Bokungu.

“Nafurahia kufunga, japokuwa ni kiungo lakini napenda kufanya hivyo, kwa staili ninayocheza na majukumu yangu yalivyo, yananiruhusu nacheza maeneo ambayo mpira unapatikana kwa wakati huo, yaani ‘box to box midfielder’ ndiyo maana nimeweza kufunga mabao ndani ya 18, sasa kwa staili hiyo nafikiri itakuwa ni kawaida yangu kufunga katika mechi zijazo.


“Ukiangalia pia mimi binafsi napenda kuisaidia timu yangu kufunga mabao, kwa hiyo ninapopata nafasi na ukizingatia majukumu yangu yalivyo uwanjani nitakuwa nafunga sana kila ninapopata nafasi ya kufanya hivyo,” alisema Mzamiru aliyetua Simba msimu huu akitokea Mtibwa Sugar.  

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV