BARTHEZ |
Pamoja na mara kwa mara Ally Mustapha ‘Barthez’ kuonekana kutokuwa makini awapo langoni, lakini hilo lisikufanye uamini kwamba hafai kwani takwimu zinaonyesha yeye na mwenzake, Deogratius Munishi ‘Dida’ wamecheza mechi sawa kwenye kikosi chao cha Yanga huku kila mmoja akilinda vilivyo lango lake.
Barthez na Dida kila mmoja msimu huu amecheza mechi tano za ligi ndani ya kikosi hicho katika mechi kumi za Yanga na kufanikiwa kuifikisha timu yao nafasi ya pili kwa kujikusanyia pointi 21.
Barthez ambaye kwa sasa anauguza majeraha ya kidole aliyoyapata kwenye mchezo wao dhidi ya Simba, Oktoba Mosi, mwaka huu walipotoka sare ya bao 1-1, katika mechi zake tano hakuruhusu bao (clean sheet) mara tatu, sawa na Dida, lakini tofauti yao ni kwamba Barthez ameishuhudia Yanga ikifungwa mchezo mmoja, huku Dida akiwa bado hajapoteza mechi hata moja.
Dida alianza kudaka msimu huu ambapo mechi ya kwanza ilikuwa dhidi ya African Lyon ambapo Yanga ilishinda 3-0 kwa mabao ya Deus Kaseke, Simon Msuva na Juma Mahadhi.
Baada ya mechi hiyo, Dida hakuonekana tena langoni kutokana na kukumbwa na msiba wa baba yake, nafasi yake aliichukua Barthez, lakini Dida alikuja kuonekana tena kwenye mchezo wa saba dhidi ya Mtibwa ambapo Yanga ilishinda mabao 3-1. Wafungaji wakiwa ni Obrey Chirwa, Msuva na Donald Ngoma, huku Mtibwa bao lao likifungwa na Haruna Chanongo.
Kuanzia hapo mpaka juzi Jumamosi, Dida amekuwa akikaa langoni ambapo kwenye mechi hizo, matokeo yalikuwa hivi; Azam FC 0-0 Yanga, Toto African 0-2 Yanga na Kagera Sugar 2-6 Yanga.
Kwa upande wa Barthez, mechi zake tano zilikuwa hivi; Ndanda 0-0 Yanga, Yanga 3-0 Majimaji, Mwadui 0-2 Yanga, Stand United 1-0 Yanga na Yanga 1-1 Simba.
0 COMMENTS:
Post a Comment