Daktari wa Yanga, Edward Bavu alimzuia Amissi Tambwe asifanye mazoezi ya timu hiyo jana kutokana na jeraha aliloshonwa nyuzi sita kichwani kutokuwa katika hali nzuri.
Kutokana na hali hiyo, Tambwe, straika raia wa Burundi, hakufanya mazoezi, hivyo kesho Jumapili hatacheza mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam FC, licha ya mwenyewe kutaka kucheza mchezo huo.
Tambwe aliumia katika mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar Jumatano wiki hii kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam dakika 88 na kushindwa kumalizia mechi hiyo iliyoisha kwa Yanga kushinda mabao 3-1.
Bavu amesema Tambwe ataukosa mchezo huo kutokana na maendeleo ya jeraha lake kwenye sehemu aliyoshonwa nyuzi sita.
Bavu alisema, kwenye mazoezi ya leo (jana), Tambwe aliomba kushiriki ili acheze mechi na Azam, lakini baada ya kumfanyia uchunguzi mdogo akaona bado kidonda chake hakijapona.
“Siioni sababu ya ‘kuriski’ maisha ya mchezaji wetu kwa kucheza mechi na Azam wakati timu ina kikosi kipana chenye wachezaji wengi wenye uwezo wa kucheza nafasi yake.
“Hivyo, kama daktari nimeshauri Tambwe akae nje ya uwanja akiendelea kuuguza majeraha yake hadi atakapopona kabisa kwani ataanza mazoezi wiki ijayo,” alisema Bavu.
Kwa upande wake, Tambwe alisema “Nilikuwa ninaitaka sana mechi ya Azam, lakini imeshindikana kutokana na jeraha hili, nimeumia kuikosa mechi hii kubwa yenye historia.”
0 COMMENTS:
Post a Comment