October 28, 2016KIGANJA

Na Saleh Ally
HIVI karibuni kumekuwa na gumzo kubwa kuhusiana na suala la mabadiliko katika klabu kubwa kongwe za Yanga na Simba.

Yanga walikuwa wamekodisha timu na nembo kwenye Kampuni ya Yanga Yetu Ltd inayomilikiwa na mwenyekiti wao, Yusuf Manji huku Simba wakijiandaa kumuuzia hisa asilimia 51 za umiliki mfanyabiashara Mohammed Dewji, maarufu kama Mo.

Wanachama wa klabu zote za Yanga na Simba, walikubaliana na ukodishwaji, pia uuzaji wa hisa hizo wakionyesha wazi wanataka kupiga hatua, kutoka walipo, lakini kukaibuka na figisu nyingi ambazo unaziona hazikuwa na msingi.

Inawezekana waliokuwa wakipinga ni robo ya asilimia moja, lakini wakaonekana wana nguvu sana kitu ambacho kilikuwa kinashangaza. Hata Baraza la Michezo la Taifa (BMT) lilipoingilia, lilisema ufuatwe mchakato lakini asilimia kubwa ya mambo iliyotaka yafanyike, yalikuwa yameshafanyika.

BMT ni mwakilishi wa serikali michezoni, nafikiri kuna haja ya kubadili njia kama ambavyo nimewahi kusema na wakaamua kuifanya michezo iwe michezo inayokwenda kwa ajili ya maendeleo na si siasa.

Barua ya BMT kusitisha mchakato huo wa Simba na Yanga, haina maelezo ya kutosha na inajikanganya. Mfano, inaeleza kuna vifungu vifuatwe kupitia kwa msajili, lakini mwisho inasema wafanyabiashara hao wakitaka waanzishe timu zao kama Bakhresa.

Sidhani kama dunia hii inaweza kwenda hivyo, kwamba kila anayetaka lazima aanzishe timu yake, ndiyo maana napata hofu ya uelewa wa michezo wa BMT au wahusika wengine. Kwamba ukitaka kuwekeza anzisha timu yako.

Manchester United, Arsenal, Chelsea na timu nyingine maarufu duniani, zina wawekezaji ambao walikuta zimeanzishwa. Hawakuanzisha timu zao na ingewezekana.

Kuna suala la biashara, kuna suala la faida lakini kuna mtaji wa watu. Manji angeweza kuanzisha Yanga Yetu FC na bado angepata mashabiki, Mo angeanzisha Simba One pia angepata watu, lakini suala la uhusiano, historia na kuwekeza kwenye biashara linabaki palepale.

Kuzuia uwekezaji linaweza kuwa jambo jema kama ilivyoamua serikali, lakini kwa kuwa lengo ni kuwasaidia wapenda michezo na wamiliki wa Yanga, vizuri tukaelezwa faida yake ni zipi na serikali sasa ijipambanue kuendeleza michezo.

Yanga haikuwa inanunuliwa, haikuwa imeuza timu, nembo wala klabu. Ilikuwa inakodishwa, imeonekana vibaya. Sasa inarudi kama zamani, kuendelea kuukalia uchumi, tafadhali serikali isaidie.
Hizi timu ni mtaji lakini zipo tu, zinatumika kwenye migogoro na faida ya wachache. Zinatumika kama sehemu ya baadhi kulia wana mapenzi nazo na wanaendelea kuchuma kiujanjaujanja.
Waliokuwa wanataka kuwekeza au kukodi wangekuwa makini, wangezipa maendeleo. Wanayanga na Wanasimba wangefurahi zaidi, serikali ingepata kodi ya juu kutokana na mapato na Bendera ya Tanzania ingepata heshima kimataifa pia.
Sasa kuziacha zibaki zilipo, bila hata ya kusema lolote itakuwa inatia hofu kama kweli BMT inataka maendeleo ya michezo kwa kuwa hata yenyewe kama mwakilishi wa serikali, imekuwa ni mshiriki duni kwa miaka nenda rudi.
Michezo ya shule za sekondari na msingi, nayo ilisitishwa kwa kuwa fedha ni kidogo, ikaonekana bora kununua madawati. Huku ambako kuna watu wamejitokeza kuwekeza nako inaonekana kuweka kauzibe.
Ninaanza kuhoji hapo kama kweli serikali ina mipango ya maendeleo ambayo ni madhubuti hasa au itakuwa inaishia tu kuzuia, kukataza na kukosoa bila ya kutoa mipango, kusaidia uwekezaji na kadhalika.

Pongezi kwa Rais John Pombe Joseph Magufuli kupitia uamuzi wake wa kumuomba Mfalme wa Morocco kuijengea Tanzania uwanja wa michezo ambao utajengwa Dodoma. 

Niweke msisitizo, michezo pia ni ajira na uwekezaji mkubwa. Vizuri serikali pia iangalie mara mbili kwamba, unahitajika uwekezaji kupiga hatua hata kama si Manji na Mo, bado hakuna hatua itapigwa kutoka tulipo, kama zitaendelea kubaki zilivyo, mwisho tutaziua kama ilivyo kwa SC Villa ya Uganda, AFC Leopards ya Kenya na wakongwe wengine.1 COMMENTS:

  1. Nina shaka kubwa na huyu Katibu mkuu wa BMT kuwa kuna watu wanamtumia kwa maslahi yao binafsi kiasi anashindwa hata kujitafakari. Ni aibu kubwa kwa mtendaji mkubwa kama yeye ( na wasiswasi na maadili yake) kutoa matamshi eti kwa wanaotaka kukodi au kumiliki hisa katika timu hizo waanzishw timu zao kama Bakhressa) haya sio matamshi ya mtu anaeijua tasnia nzima ya michezo na hasa Football. Iwapo kila mtu ataanzisha timu yake tutaua soka la Tanzania maana hakutakuwa na ushindani wa kweli. NAOMBA MAMLAKA ZILIZOMTEUA ZIANGALIE UPYA SIFA ZA MUHUSIKA.

    ReplyDelete

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV