October 5, 2016

STAND UNITED
Vikosi vya Mbeya City na Stand United vimechimbana mkwara mzito kila upande ukitamba kuibuka na ushindi katika mchezo unaotarajiwa kupigwa Jumamosi hii huko mkoani Mbeya.

Timu hizo zinakutana zikiwa na jeuri ya kuibuka na ushindi katika michezo yao ya mwisho ya ligi msimu huu, ambapo City iliifunga Mwadui kwa bao 1-0 na kukamata nafasi ya saba ikiwa na pointi 11, Stand ikaitungua Majimaji mabao 2-0 na kufikisha pointi 15, ikiwa nafasi ya pili, nyuma ya kinara Simba mwenye 17.

Ofisa Habari wa Stand, Deo Makomba, ameeleza kuwa hawana wasiwasi na mwendo walionao sasa, wamepania kumfunga kila watakayekutana naye ingawa wanajua Mbeya City ni timu ngumu lakini wataichapa hukohuko kwao.

“Cha msingi waamuzi wawe ‘fair’ tu na watende haki lakini kuhusu kikosi chetu tunakiamini na benchi la ufundi lipo vizuri, mchezo hautakuwa mwepesi lakini tumepanga kushinda katika kila mchezo ulio mbele yetu, maana nia yetu ni kuhakikisha tunamaliza katika nafasi tatu za juu msimu huu,” alisema Makomba.

Kwa upande wa Ofisa Habari wa City, Dismas Ten, alisema: “Tunachokitaka siku zote ni ushindi na ukizingatia tupo nyumbani, kwa hiyo tumejizatiti ingawa mpira ni dakika 90, hizo zitaamua nani mshindi baada ya mchezo. Timu itaanza maandalizi (jana) leo jioni tayari kwa ajili ya mchezo huo.”


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV