October 26, 2016


LWANDAMINA
Uliisikia hii? Imefahamika Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) limemzuia Kocha Mkuu mtarajiwa wa Yanga, Mzambia, George Lwandamina kusaini mkataba wa kukinoa kikosi hicho huku akitimkia kwao jana usiku.

Mzambia huyo mwenye mkataba na Klabu ya Zesco ya Zambia, alitua nchini hivi karibuni kwa ajili ya kusaini mkataba wa kuifundisha Yanga akichukua nafasi ya Mholanzi, Hans van Pluijm aliyeusitisha mkataba wake wa mwaka mmoja wa kuendelea kukinoa kikosi hicho.

Pluijm alifikia maamuzi hayo ya kusitisha mkataba wake baada ya kupata taarifa ya ujio wa Lwandamina aliyetua nchini wikiendi iliyopita.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo Championi Jumatano limezipata, uongozi wa Yanga na kocha huyo wamefikia muafaka mzuri, lakini ameshindwa kupewa mkataba kwa hofu ya kuvunja kanuni na sheria za Fifa ambazo hazimruhusu mchezaji na kocha kusaini mkataba akiwa tayari anao wa klabu nyingine kama ilivyo kwa Lwandamina.

Mtoa taarifa huyo alisema, Lwandamina bado ana mkataba na Zesco, hivyo uongozi umemtaka kwenda kumalizana haraka na klabu hiyo kabla ya kurejea nchini baada ya wiki moja kuja kusaini mkataba wa kuifundisha Yanga.

Aliongeza kuwa, kocha huyo ameahidi kurejea nchini Oktoba 31, mwaka huu kwa ajili ya kusaini mkataba huo na kesho yake Novemba Mosi anatarajiwa kuanza kibarua cha kukinoa kikosi hicho akiwa tayari amemalizana na Zesco.

“Taarifa nyingi zimezagaa kuwa Lwandamina amesaini mkataba wa miaka miwili wa kuifundisha Yanga, kiukweli hizo taarifa ni za uongo mtupu, ilikuwa ni ngumu kwetu kumsainisha mkataba kocha huyo akiwa bado ana mkataba na Zesco.

“Kanuni za Fifa zipo wazi, kumsainisha mchezaji au kocha akiwa ndani ya mkataba na makosa, hivyo hatutaki kukutana na adhabu zisizokuwa na msingi kutoka Fifa, hivyo tumemwambia kocha huyo arejee nyumbani kwao kwa ajili ya kumalizana na klabu yake ya Zesco.

“Kikubwa tunashukuru kuwa, mazungumzo yetu na yeye yameenda vizuri kwa kukubaliana baadhi ya vitu ikiwemo mshahara na fedha ya kumtoa Zesco na kumleta Yanga.
“Hivyo Lwandamina anatarajiwa kurejea tena nchini baada ya wiki moja na siku hiyohiyo atasaini mkataba na kesho yake Novemba Mosi, basi ataanza kibarua cha kuifundisha Yanga,” alisema mtoa taarifa huyo.


Alipotafutwa Katibu Mkuu wa timu hiyo, Baraka Deusdedit kuzungumzia hilo, alisema: “Lwandamina bado hajasaini mkataba wa kuifundisha Yanga, ni vema hilo likajulikana na ikumbukwe kuwa, huyo kocha ana mkataba na Zesco.”

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV