October 12, 2016Kocha Mkuu wa Simba, Mcameroon, Joseph Omog, amewataka washambuliaji wake, Laudit Mavugo na Ibrahim Ajibu kuhakikisha wanaiwezesha timu hiyo kuibuka na ushindi dhidi ya Mbeya City, leo.

Kocha huyo amesema wachezaji hao wanatakiwa kuhakikisha wanafanya kama kiungo mshambuliaji wa timu hiyo Shiza Kichuya alivyofanya kwenye mchezo dhidi ya Azam na Yanga.

Leo jioni timu hizo mbili zinashuka uwanjani katika mchezo wa Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, ambapo Simba itakuwa ikihitaji ushindi ili izidi kujichimbia juu katika msimamo wa ligi hiyo wakati Mbeya City nayo inahitaji matokeo mazuri ili iweze kujitengezea mazingira mazuri kwenye ligi hiyo.

Omog alisema kuwa ufanisi mzuri wa Mavugo na Ajibu ambao wamekuwa wakiuonyesha mazoezini katika kuzifumania nyavu hivi karibuni, wanatakiwa kuuonyesha uwanjani leo kama ambavyo Kichuya amekuwa akifanya kwa sababu wao ndiyo washambuliaji anaowategemea kwa kufunga.

Katika mechi mbili zilizokuwa na ushindani mkubwa ambazo Simba ilicheza hivi karibuni dhidi ya Azam na Yanga, Kichuya ndiye mchezaji aliyeifungia timu hiyo mabao ambayo yaliwezesha kujikusanyia pointi tatu kwenye mechi hizo ambazo Ajibu na Mavugo walishindwa kuonyesha makeke yao.

“Namshukuru Mungu mpaka sasa hakuna majeruhi yeyote katika kikosi changu, wachezaji wote wapo vizuri ila nimewaambia kuwa nataka ushindi katika mchezo huu.
“Mavugo na Ajibu pia nimewaambia wapambane vilivyo kuhakikisha tunashinda kwa sababu wao ndiyo washambuliaji tunaowategemea.

“Nafikiri wanatakiwa kuonyesha kasi nzuri sana kwenye mchezo huu,” alisema Omog.

SOURCE: CHAMPIONI


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV