October 28, 2016

LWANDAMINA


Na Saleh Ally
HAKUNA ambaye anaweza kusema hakushituka au kushangazwa na kuona Kocha Hans van der Pluijm akiondoka, tena katika kipindi Yanga imeamka na kuanza kufanya vizuri.

Uongozi wa Yanga, umeamua kumleta Kocha George Lwandamina na kufanya naye mazungumzo. Mzambia huyo kutoka Zesco ya Zambia, alitua nchini na baada ya kumalizana na Yanga akaondoka.

Kuondoka kwa Pluijm, hakuwezi kushangaza sana kama utaangalia mambo mengi yanayohusu mpira na makocha walioondoka katika timu mbalimbali iwe Ulaya au hapa.

Mfano mzuri unaweza kuwa ni ule wa Yanga wakati makocha kadhaa walioondoka walionekana wanaweza au wanafanya vizuri lakini wakaondoshwa. Wako waliofanya vizuri zaidi walipokwenda na wako waliofeli, hayo ndiyo maisha ya mpira.

Sam Timbe raia wa Uganda aliondoka Yanga, Oktoba 2011, akiwa anafanya vizuri tena baada ya kuipa timu hiyo ubingwa wa Kombe la Kagame, kumbuka aliifunga Simba chini ya Mganda mwingine, Moses Basena.

Alifuatia Mbelgiji, Tom Saintfiet naye akaipa ubingwa wa Kagame, hakudumu hata kwa siku 100 naye akaondoka na nafasi yake kuchukuliwa na Mholanzi Ernie Brandts ambaye alikuwa na mafanikio kwa kuipa Yanga ubingwa mara mbili.

Kama unakumbuka, kipigo cha mabao 3-1 katika mechi ya Bonanza la Nani Mtani Jembe. Brandts naye akatupiwa virago, hakuna aliyeamini. Tangu Timbe, Saintfiet, Brands lilikuwa ni suala la kutoamini kinachotokea.

PLUIJM
Kocha ambaye alichukuliwa baada ya Brandts, Marcio Maximo ndiye pekee alifeli katika mfumo huo wa makocha kuondolewa Yanga kwa kushitukizwa. Waliobaki kila aliyeingia alifanya kazi yake vizuri.

Mimi nilijua Maximo atafeli na nilieleza mapema, sikuwa ninamaanisha ni kocha mbaya lakini Yanga imebadilika na inataka mafanikio kwa kasi ya juu na si kujiandaa taratibu kama ambavyo alifanya Maximo kwenye kikosi cha Taifa Stars.

Yanga ina haraka, inataka mambo fasta na kocha anayekuja anatakiwa kuanza kuleta matokeo, hakuna haja ya kujipanga. Hilo pia linawezekana kwa Yanga kwa kuwa mara nyingi, kila kocha anayejiunga nayo anakuta ina wachezaji wa ushindani na wanaoweza kusaidia kupatikana kwa matokeo.

Kama Yanga itamalizana na Lwandamina, basi hakuna shaka ukijumlisha rekodi zake kikazi na Yanga ilivyo sasa, ataendelea kufanya vizuri lakini ni lazima aungwe mkono na Wanayanga wenyewe.

Yanga wanachopaswa kwa sasa ni kufanya mambo mawili makubwa ambayo yataifanya timu yao iendelee kufanya vizuri katika mwendo ambao amewaachia Pluijm.

Kwanza, kumuonyesha Pluijm mapenzi, wamalizane naye vizuri na kumpa heshima yake kutokana na kazi yake nzuri ambayo amewafanyia na upendo alioonyesha. Mseme: “Ahsante Pluijm”.

Jambo la pili kubwa ni kumkubali, kumpokea na kumuunga mkono kocha ajaye kama atakuwa ni Lwandamina au mwingine. Maana ndiye atakuwa kocha wao, kocha wa timu yao ambaye anakiongoza kikosi chao.

Kama Yanga watataka kufeli, basi waendelee kulia na kupiga kelele kuhusiana na Pluijm ambaye ameamua kujiuzulu na kuendelea na maisha yake mengine. Halafu wasubiri kumlaumu au watamani Lwandamina au kocha mwingine atakayekuja afeli, hapo itakuwa ni kujifelisha wenyewe.

Yanga walimshukuru Timbe, wakamuunga mkono Saintfiet, wakamshukuru Saintfiet wakamuunga mkono Brandts. Ulipofika muda, naye wakamshukuru pia na kumuunga mkono Pluijm.

Huu ni wakati kwao kumuunga mkono kocha ajaye kwa ajili ya Yanga kwa kuwa ndiye atakuwa anaongozana nao na kupambana kwa ajili ya kuwaleta mafanikio. Wakimfanya adui au wasiyemtaka, basi ni sawa na mwanadamu kukataa moja ya kiungo cha mwili wake wakati kinamsaidia kusimama, kuzungumza, kuona au kupumua.

Maisha ya soka ni mzunguko, hauwezi kujua lini Pluijm ataisaidia tena Yanga, huwezi kujua kocha ajaye atakuwa na faida na Yanga kwa kiasi gani. Hivyo maneno ya lawama, yasipewe nafasi ili tuendelee kujifunza.


Kama kocha mpya atapewa ushirikiano, halafu akafeli mwenyewe. Kila kitu kitaonekana kwa kuwa mpira hauchezwi chumbani. Basi hapo, haki ya wanachama kusema kwa nia ya kujenga, isiminywe, ili mradi mjadala uwe unaosaidia kujenga pia.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV