November 7, 2016


Bondia wa ngumi za kulipwa nchini, Abdallah Pazi ‘Dulla Mbabe’, juzi Jumamosi alijikuta akipoteza pambano lake la Ubingwa wa Dunia (WBC) dhidi ya Mjerumani Toni Kraft licha ya kudaiwa kumpiga mpinzani wake vya kutosha.

Katika pambano hilo la raundi kumi lililofanyika kwenye Ukumbi wa Ballhaus Forum, Munich, Ujerumani, Mbabe alionekana kumdhibiti vilivyo Mzungu huyo kwa kumpelekea makonde mazito kabla ya kumdondosha chini katika raundi ya tatu kufuatia kumchapa konde kali la mkono wa kulia, hali iliyosababisha ahesabiwe mpaka kumi lakini aliweza kuokolewa na kengele ya mapumziko.

Baada ya kipondo hicho, Mzungu huyo alianza kucheza kwa kukimbia muda mwingi ulingoni huku akipokea ‘vikombe’ kutoka kwa Dullah Mbabe hadi kumaliza raundi kumi na majaji wawili kumpa ushindi Mjerumani huyo hali iliyosababisha mashabiki waliojitokeza kwenye pambano hilo kuamini kuwa Mzungu mwenzao hakustahili kushinda pambano hilo.

Akizungumza mara baada ya pambano hilo moja kwa moja kutoka katika Jiji la Munich, Ujerumani, Mbabe alisema amesikitishwa na matokeo hayo, kwani majaji walimpendelea mpinzani wake, licha ya kumpiga katika raundi zote.

“Kiukweli nimepoteza pambano langu kimizengwe, majaji wamempa mpinzani wangu ushindi wa jumla kwa tofauti ya pointi mbili, kitu ambacho kimepingwa hata na mashabiki wa ngumi huku Ujerumani, wengi wao ni Wazungu, kwa kuwa kila mtu ameona nilivyokuwa namshughulikia bondia wao.


 “Nilimpiga ngumi kali ya kulia akaenda chini lakini alihesabiwa mpaka nane na akaweza kuendelea na pambano kwa ujanja kwani muda mwingi nilikuwa nampa vitasa vizito,” alisema Mbabe.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV