November 19, 2016


Mwadui FC ya Shinyanga ipo nafasi ya 15 katika Ligi Kuu Bara ambayo ni moja kutoka mkiani, eti straika wake Jerry Tegete amesema hataiacha timu hiyo hadi ahakikishe anaipa ubingwa.

Tegete, tofauti na nyota wengine wa ligi hiyo ambao wamewahi kucheza Simba au Yanga ambao mara nyingi wanapoona jahazi linazama hukimbia, amesema anakomaa na Mwadui hadi mwisho.

Straika huyo wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, hadi sasa ameifungia Mwadui mabao mawili kati ya michezo 12 iliyonayo na kuiwezesha kuwa na pointi 13 ambapo imecheza mechi 15, imefungwa mara nane, imeshinda mara tatu na kutoka sare nne.

Tegete amesema kuwa: “Sitaikimbia Mwadui, nakomaa hapa hadi nione imepata nafuu, ningependa kuondoka baada ya kutwaa ubingwa wa ligi kuu au timu kufika katika nafasi nzuri.

“Mwadui msimu uliopita walinivumilia msimu wote nikiwa benchi nauguza goti langu na sasa nipo vizuri, nitakuwa mtovu wa nidhamu kama nimepona halafu nianze mipango ya kuachana na timu yangu.

“Bado naipenda Mwadui na wala haijawahi kunikosea kwa namna yoyote iwe kwa uongozi au kwa wachezaji wenzangu, hivyo siendi popote,” alisema Tegete ambaye baba yake Mzee John Tegete ni Mkurugenzi wa Ufundi wa Alliance FC ya Ligi Daraja la Kwanza.

Mwadui haina mwenendo mzuri katika ligi kuu tofauti na msimu uliopita, hali hiyo ilianza kabla ya Kocha Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ hajaamua kuondoka na nafasi yake kuchukuliwa na Khalid Adam.


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV