November 14, 2016


Pamoja na kuaga kuondoka, Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van Der Pluijm amegoma kumpisha George Lwandamina katika ardhi ya Bongo na ameweka wazi kuwa bado yupo sana nchini akiwa na mkewe kwa ajili ya kupumzisha akili yake.

Kocha huyo, Jumanne iliyopita katika mazoezi ya mwisho ya kujiandaa na mechi dhidi ya Ruvu Shooting aliwaaga wachezaji wa timu hiyo huku nafasi yake ikichukuliwa na Mzambia, George Lwandamina ambaye yupo nchini tangu Jumatano iliyopita na ameshasaini mkataba wa miaka miwili kimyakimya huku viongozi wakiendelea kuwazuga wanachama kwa kukana hadi pale watakapokuwa tayari kumtambulisha.

Mholanzi huyo, mechi dhidi ya Ruvu ilikuwa ya mwisho kwake kukaa kwenye benchi na kufanikiwa kupata ushindi wa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Pluijm amesema haoni sababu ya kuondoka hivi sasa kutokana na mke wake kuwepo nchini wiki ya pili sasa akitokea nyumbani kwao Ghana wanapoishi.
Pluijm alisema mwaka huu hawakupata nafasi ya kupumzika na familia zao kutokana na kubanwa na michuano ya kimataifa iliyokwenda sambamba na msimu mpya wa Ligi Kuu Bara, hivyo amepanga kupumzisha akili yake hapa nchini kwa kula bata na mke wake.

“Kama ulivyokuwa unaona ratiba ilivyokuwa inatubana mwaka jana na huu, tulikosa muda wa kupumzika kabisa tofauti na timu nyingine kutokana majukumu ya michuano ya kimataifa.

“Hivyo, huu ni muda muafaka kwangu kupumzisha akili na kufurahia maisha na mke wangu ambaye amekuja tangu wiki iliyopita, hivyo nipo naye nchini kwa ajili ya mapumziko huku nikiweka sawa mambo yangu binafsi,” alisema Pluijm.


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV