November 7, 2016
Na Saleh Ally
TANZANIA haina maendeleo makubwa sana katika mchezo wa soka, lakini ina watu ambao wana historia kubwa kama utazungumzia mpira wa nchi hii.

Huenda kungekuwa na watu wenye historia kubwa hasa unapozungumzia mafanikio. Mfano ungeweza kuwataja wanariadha watatu, Filbert Bayi, Juma Ikangaa na Suleiman Nyambui lakini wako wengine wengi.

Hawa wachache waliopo, nao wameshindwa kuuinua mchezo wa riadha kwa kuwa wengi wao pia hawaelewani, wanalaumiana na wengine wakisema wenzao wanautumia mchezo huo kwa maslahi yao binafsi.

Katika soka, wengi wa magwiji au wakongwe, baada ya kustaafu kucheza soka wamekuwa wakiendelea na maisha yao kama kawaida na si ndani ya soka.

Wapo baadhi wanajitahidi kushiriki katika mambo kadhaa ya mchezo huo lakini si kama vile ambavyo leo unawaona viungo wa zamani wa Real Madrid, Zinedine Zidane na Pep Guardiola wanavyofanya vizuri huku wakichota mishahara ya mamilioni ya fedha.

Magwiji wa soka wa hapa nyumbani ni wale watu walioamua kukaa kimya kuhusiana na vitendo kwenda kwenye mabadiliko au kwenda kwenye maendeleo katika michezo.

Badala yake, wengi wao wamekuwa wakilaumu sana kwamba wametengwa, wamesahauliwa na inaweza kuwa na klabu walizozichezea au serikali. Wao ili mradi wanakuwa na mtu wa kumlalamikia.

Wengi hulalamika kwamba wamesahaulika, hakuna anayewajali, lakini wao pia hawaujali mchezo wa soka na hawakuwa na maandalizi wakati wanatarajia kustaafu.

Kawaida hasa Ulaya, wachezaji wengi huanza mafunzo ya ukocha wanapokuwa katika hatua za mwisho za miaka yao ya uchezaji.

Huku wanacheza, taratibu wanapata nafasi ya kuchukua mafunzo ya kocha wa watoto, kocha wa vijana, kocha msaidizi na mwisho wanakuwa makocha wakuu.

Maandalizi haya hufanyika kwa muda mrefu na wanaofanya hufanya wakiwa wanajua wamelenga nini mapema kabisa. Ndiyo maana wanapostaafu baada ya muda unasikia wana nafasi ya kuzinoa timu fulani.

Mfano pale Real Madrid, baada ya Zinedine Zidane kuwa ameandaliwa, sasa maandalizi yapo kwa Jose Maria Gutirez maarufu kama Guti. Huyu anaendelea kuzinoa timu za vijana za Madrid.

Maana yake, siku moja utasikia yeye ni kocha msaidizi na siku nyingine anaweza kuwa kocha mkuu kama ambavyo imeamua kufanya Real Madrid kwa Zidane.

Mabadiliko katika michezo duniani yamekuwa na kasi kubwa ambayo inatuacha sisi. Wanamichezo wetu bado wameganda kwenye hisia za mambo yale ya zamani na mfumo huo wa wakati huo.

Kila mmoja anaamini baada ya kustaafu kucheza soka, basi anaanza kuitumikia timu moja ya veterani na maisha ndiyo yanakuwa yamefikia tamati. Kweli si rahisi watu wote kuwa makocha lakini tukubaliane, wanamichezo wanatakiwa kuendeleza michezo.

Kuiendeleza si lazima kila mmoja ashinde kwenye uongozi tu. Maendeleo yanaweza kuletwa na mtu ambaye yuko nje ya uongozi, mfano kocha ambaye ni mchezaji mkongwe akawa anawafundisha vijana wanaofanya vizuri.

Tabia ya kulalamika katika mambo mengi sana imetuangusha Watanzania. Huenda kupitia mabadiliko katika mchezo tunaweza kubadilika na kuachana na kuabudu sana masuala ya kulalamika kila wakati.

Mkongwe anayestaafu lazima atakuwa na watoto au watoto wa ndugu au rafiki yake ambao wanashiriki michezo na wangehitaji uzoefu wake ndani ya michezo na pia kipaji chake.

Hivyo lazima wakongwe wakubali badala ya kulalamika sana, basi suala hili lilalie kwenye kutenda sana na kusaidia maendeleo ya mchezo wa soka na michezo mingine pia.


Mkongwe wa soka hapaswi kulalamika ametengwa na hapewi nafasi ya kuchangia kusukuma gurudumu. Badala yake anatakiwa kuonyesha anaweza kusaidia na anahitaji kufanya hivyo na mambo yanawezekana.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV