Kiungo kwenye kasi wa Yanga, Simon Msuva, amewajibu wale wanaomfananisha na winga wa Simba, Shiza Kichuya, kwamba yeye si wa levo hizo, labda wamfananishe na Ramadhan Singano ‘Messi’ wa Azam.
Msuva ameyasema hayo baada ya kusikia kelele za mashabiki zikimfananisha na kumshindanisha na Kichuya ambaye anaongoza kwa ufungaji katika Ligi Kuu Bara akiwa na mabao tisa huku Msuva akiwa na mabao sita.
Msuva alisema wanakosea sana wanaomfananisha na Kichuya kwani hawafanani hata kidogo kutokana na kwamba Kichuya ameibuka hivi karibuni wakati yeye kitambo anatesa katika ligi.
“Mimi nipo juu zaidi yake, wanaonifananisha naye wanakosea tena sana, labda kidogo wanifananishe na Singano ambaye hakuna asiyeufahamu uwezo wake tangu hapo awali.
“Huyo Kichuya wa juzi tu, najua anaongoza kwa ufungaji akiwa na mabao tisa, lakini mimi pia sipo mbali naye, nimefunga mabao sita, nimetengeneza mabao 13 msimu huu, sasa yeye katengeneza mangapi? Waache kutufananisha bwana,” alisema Msuva.
Wakati Msuva akisema ametengeneza mabao 13 na kufunga sita mpaka sasa, kwa upande wa Kichuya takwimu zinaonyesha kwamba mbali na mabao yake tisa yanayomuweka kileleni, lakini ametengeneza mabao mawili tu.
0 COMMENTS:
Post a Comment