November 9, 2016


Pamoja ya kupokea kichapo cha mabao 2-1 dhidi ya Ndanda FC ya mkoani Mtwara, Kocha wa Stand United, Athuman Bilali, ameelezea kuwa waokotoa mipira walikuwa wakiificha ili kupoteza muda.

Timu hiyo imepoteza mchezo wake wa pili kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara lakini kocha huyo amesema mechi hiyo ilikuwa na madudu mengi kama siyo ya Ligi Kuu Bara.

Stand ambayo tayari imeshamaliza mzunguko wa kwanza wa ligi kwa kuwa nafasi ya tano na pointi 22, ilicheza mchezo wake wa mwisho dhidi ya Ndanda ya Mtwara na kupokea kichapo cha mabao 2-1.

Bilali amesema wamejikuta katika wakati mgumu kwenye mchezo huo kufuatia waokota mipira kushirikiana na mashabiki katika kuficha mipira huku mechi ikiwa inaendelea ikiwa ni pamoja na kuchelewesha muda.

“Kwa kweli mechi tuliyocheza na Ndanda hatukucheza muda mwingi kutokana na mipira kufichwa na waokota mipira ambapo walikuwa wanatumia muda mwingi kuitoa kwa lengo la kupoteza muda.

“Wakati mwingine mpira ukitoka nje mashabiki wanapiga kuelekea nje, hii ni baada ya kuona Ndanda wanaongoza kwa lengo la kupoteza muda.


“Wakati tunaanza mechi tulikuwa na mipira 10 lakini hadi mechi inakuja kumalizika tumejikuta tukiwa na mipira miwili tu ambayo ndiyo imebaki jambo ambalo si sahihi,” alisema Bilali.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV